Windows

Yanga yaifumua Azam katika uwanja wa Uhuru

Mtanange wa Ligi Kuu Tanzania Bara kati ya Azam FC na Yanga, umekamilika kwa Yanga kuibuka na ushindi wa goli 1-0 ikiwa ndio mara ya kwanza mchezo wa ushindani kufanyika Uwanja wa Uhuru baada ya kupitia matengenezo makubwa kwa ajili ya mashindano ya vijana ya AFCON yaliyofanyika Tanzania.

Ushindi wa Yanga umekuja kupitia goli lililofungwa na Mrisho Ngassa dakika ya 13 akimalizia pasi ya Ibrahim Ajibu.

Azam FC walijitahidi kufanya mashambulizi ili kusawazisha bao na kuongeza lingine lakini juhudi zao ziliishia kwa beki kiongozi kwa mechi hiyo Abdallah Shaibu ‘Ninja’.

Mpaka kipindi cha kwanza kinamalizika Yanga walikuwa mbele kwa goli moja kwa bila huku mchezo ukionekana kuwa sawa kwa maana ya mashambulizi.

Kunako kipindi cha pili, kocha wa Yanga SC, Papaa Mwinyi Zahera raia wa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo aliimarisha safu ya ulinzi kwa kumtoa Ajibu na kumuingiza kiungo wa ulinzi, Said Juma ‘Makapu’. Washambuliaji wa Azam FC, Donald Ngoma, Obrey Chirwa na Daniel Lyanga pamoja na kiungo Mudathir Yahya wote walikosa mabao ya wazi leo.

Kwa ushindi huo, Yanga SC inafikisha pointi 77 baada ya kucheza mechi 33 ikiendelea kuongoza Ligi Kuu mbele ya mabingwa watetezi, Simba SC wenye pointi 69 baada ya mechi 27, wakati Azam FC inabaki nafasi ya tatu na pointi zake 66 za mechi 33.

Vikosi vya timu zote mbili vilikuwa hivi

Yanga SC; Klaus Kindoki, Paul Godfrey, Gardiel Michael/Jaffar Mohammed dk38, Andrew Vincent ‘Dante’, Abdallah Shaibu ‘Ninja’, Feisal Salum, Mrisho Ngassa, Mohammed Issa ‘Banka’, Heritier Makambo, Ibrahim Ajibu/Said Juma ‘Makapu’ dk76 na Raphael Daudi.

Kikosi cha Azam FC kilikuwa; Razack Abalora, Nicolas Wadada, Bruce Kangwa, Lusajo Mwaikenda, Yakubu Mohamed, Stephan Kingue, Joseph Mahundi/Ennock Atta-Agyei dk76, Mudathir Yahya, Donald Ngoma, Obrey Chirwa na Salum Abubakar ‘Sure Boy’.


Post a Comment

0 Comments