Windows

Yanga kumenoga! Wachezaji kulamba posho Sh120 Mil, Zahera apelekewa maagizo mazito



Yanga kwa sasa inaongozwa na kamati za mpito hadi hapo uchaguzi utakapofanyika Aprili 28, mwaka huu, lakini jambo la kufurahisha ni kuwa kamati hizo zinaongozwa na watu wenye uwezo wao kifedha na wana taalamu mbalimbali.


Juzi, Yanga ilikata tiketi ya kucheza nusu fainali ya Kombe la FA kwa kuichapa Alliance kwa mikwaju ya penalti kwa 4-3 huku baadhi ya mabosi wa kamati hizo wakiwa jukwaani.



Baada ya mchezo huo, matajiri hao wakakutana na wachezaji na kutangaza kutenga bajeti maalumu kwa ajili ya kuhakikisha wanabeba ubingwa wa Ligi Kuu Bara na ule wa FA.
Katika kuonyesha kuwa wako siriasi na hawatanii, matajiri hao wakatangaza kwa wachezaji kuwa kila mechi watakayoshinda watapewa posho ya Sh 10 milioni fasta tu tena hata kabla ya kuondoka uwanjani. Kwa hesabu za haraka haraka wachezaji wa Yanga wametengewa bajeti ya Sh120 milioni kwa ajili ya posho kuanzia sasa.


Hapo achana kabisa na zile pesa za kunogesha shughuli zinazochangwa na wanachama viwanjani kwa staili ya kupitisha ndoo, vikao na maboksi ama zile za kwenye makundi mbalimbali ya WhatsApp, hizo ni kutoka kwa mabosi wa kamati hizo tu.


Iko hivi Baraza la Wadhamini la Yanga chini ya Mwenyekiti wake Kapteni George Mkuchika, liliunda kamati moja nzito ya kusimamia timu inayoongozwa na Lucas Mashauri. Mashauri, ambaye ndiye mwenyekiti juzi aliwakusanya wajumbe wake na kwenda Mwanza, ambako walikutana na wachezaji na kutambuana.


Katika utambulisho huo, vigogo hao akiwemo Makamu Mwenyekiti Said Ntimizi ‘Mtu mzito’, walitumia dakika 25 tu kuwapa wachezaji mikakati mizito na kuwaeleza kwamba, kila mechi ya ushindi kuna Sh 10 milioni kama posho. Hapo wachezaji mzuka ukapanda na kila mmoja kuonyesha tabasamu.


Ntimizi, ambaye ndiye alisimamia jukumu hilo, akawaeleza wazi wachezaji kuwa hakuna mkopo kwenye posho hiyo hivyo, kazi iliyobaki ni moja tu kupambana uwanjani kusaka ushindi kwenye mechi zote zilizobaki.


Ntimizi, ambaye aliambatana na wajumbe wengine akiwemo Husein Nyika naYanga Makaga wakatinga kwenye vyumba vya wachezaji uwanjani hapo kukabidhi ‘mzigo’ wa Sh 10 milioni kwa kiungo ambaye alikuwa nahodha kwenye mchezo huo, Thabani Kamusoko.


Kamusoko, ambaye kwenye mchezo huo alishtua mioyo ya mashabiki wa Yanga wakati wa upigaji penalti akitumia staili ya maarufu kwa Panenka.
Kwa sasa kwa hesabu rahisi ni kwamba, Yanga imecheza mechi 28 za ligi wakisalia na mechi 10 kumaliza ligi, lakini pia ikibakiza mechi mbili za nusu fainali na fainali kama itapenya kwa Lipuli pale Iringa, na kufanya kuwa na jumla ya mechi 12.


Kwa ahadi ya Sh10 milioni kwa kila ushindi, wachezaji wa Yanga watavuna Sh120 milioni ukiondoa 10 za juzi pale CCM Kirumba.
Ntimizi mwenyewe ameliambia Mwanaspoti kuwa, kwenye mechi kubwa na ambazo zitakuwa na umuhimu mkubwa kwa timu kupata matokeo mazuri basi mzigo huo utaongezeka.


Pia, alisema kuwa kila mechi ambayo Yanga itasafiri nje ya Dar es Salaam, itaongozana na wajumbe wa kamati yake ikiwa ni mkakati wa kuongeza mzuka na kukabidhi mzigo huo kila baada ya mchezo.


“Tunataka kutekeleza kwa vitendo jukumu letu tulilopewa na klabu na kwenye soka hakuna kitu kizuri kama hamasa kwa wachezaji wetu.
“Tumekuja hapa Mwanza kukutana na kuzungumza na wachezaji, tumewapa hiyo ahadi na tulikabidhi posho kwa ushindi dhidi ya Alliance. Tuna mikakati mingi kuhusu klabu yetu, lakini mengine ni siri za ndani kwa sasa kwani, tuko kwenye vita ya ubingwa,” alisema Ntimizi.

Post a Comment

0 Comments