Windows

Bilionea Tp Mazembe ampoteza Vibaya Mo Dewji




APRILI 6, mwaka huu Simba itakuwa kibaruani katika Ligi ya Mabingwa kwa kucheza na TP Mazembe. Mechi hiyo ni ile ya Ligi ya Mabingwa Afrika Hatua ya Robo Fainali. Mechi hiyo inatajwa kuwa kali kutokana na upinzani wa klabu hizo mbili ambapo hii mara ya kwanza kukutana kwao tangu mwaka 2011.

Nje ya mechi hii itakayopigwa Uwanja wa Taifa jijini Dar, kuna vita kubwa ya mabilionea wawili, Mohammed Dewji ‘Mo’ wa Simba na Moise Katumbi wa Mazembe. Mabilionea hawa kila mmoja amefanya mambo katika kikosi chake kwa ajili ya kukijenga. Cheki mambo ambayo wameyafanya.


MATAJI

Akiwa ndani ya Simba tangu mwaka 1999, Mo amefanikiwa kuifanya timu hiyo itwae mataji ya Ligi Kuu Bara, Kombe la Hedex na Tusker sambamba na ubingwa wa Shirikisho (FA).

Bilionea huyo pia ana rekodi ya kipekee kwa kuchangia Simba itinge hatua ya makundi ya Mabingwa Afrika kwa kumng’oa Zamalek ugenini, mwaka 2003. Mo alijiweka pembeni kabla ya kurudi hivi karibuni kuidhamini timu hiyo. Katumbi tangu mwaka 1995 ndiye mdhamini wa klabu hiyo yenye nguvu nchini DR Congo.

Chini yake TP Mazembe imetwaa kila taji ambalo wameshiriki na kugombania. Wamechukua ubingwa wa ligi zaidi ya mara 10, Ubingwa wa Kombe la Congo mara tatu, Ligi ya Mabingwa mara tatu 2009, 2010 na 2015.

Pia ubingwa wa Kombe la Shirikisho mara mbili na Super Cup mara tatu, pia Mazembe wana rekodi ya kuwa klabu pekee ya Afrika ambayo imecheza fainali ya Kombe la Dunia kwa Klabu na walifungwa na Inter Milan ya Italia mwaka 2010. Katumbi akiwa Mazembe ameifanya klabu hiyo
ichukue mataji 22 tofauti.

USAJILI

Usajili mkubwa alioufanya Mo akiwa ndani ya Simba ni ule wa bilioni 1.3 misimu miwili nyuma, jambo ambalo liliwashangaza wengi. Katika bilioni hizo 1.3 mastaa Emmanuel Okwi, John Bocco, Haruna Niyonzima, Aishi Manula na Shomari Kapombe waliwasili kabla ya msimu huu kumwaga milioni 600 na kuwanasa Claytous Chama, Meddie Kagere, Paschal Wawa, Hassan Dilunga, Adam Salamba na Deo Munishi ‘Dida’ na wengine wengi.

Wakati Simba wakitambia usajili huo wa bilioni 1.3 kwa Mazembe fedha yao ya usajili ni kubwa zaidi ya hiyo waliokuwa mastaa wao kama Rainford Kalaba, Given Singuluma, Stoppila Sunzu walichukua fedha nyingi sana.

Sasa wamebaki Wazambia kadhaa wakiongozwa na Nathan Sinkala lakini fowadi tegemeo ni Mkongo Tresor Mputu aliyerudi hivi karibuni akitokea Angola.

Ni miongoni mwa sajili za Mazembe zilichota fedha nyingi. Kwa msimu huu Mazembe wenyewe wamefanya usajili wa bilioni 4.9 ikiwa ni mara mbili ya usajili wa Simba.

BENCHI LA UFUNDI

Hapa Simba wameachwa mbali katika suala zima la ulipwaji wa benchi lao la ufundi pamoja na muundo wake. Mazembe wana benchi refu lenye wataaluma wengi zaidi wa ndani na nje ya Afrika. Aliyekuwa Kocha wa Mazembe, Hubert Velud alikuwa anakunja zaidi ya milioni 35 kabla ya kuondolewa.

Kocha wa sasa wa klabu hiyo ni Mihayo Kazembe. Kocha wa Simba, Patrick Aussems yeye anapokea Tsh 22.7mil kwa mwezi.

UDHAMINI

Mo ameweka udhamini wa kinywaji chake cha Mo Energy kwenye jezi ya Simba kwa kuingia mkataba wa udhamini wa jezi kwa mwaka mmoja wenye thamani ya Sh 250 milioni akiungana na mdhamini mkuu, SportPesa. Mazembe wenyewe wanadhaminiwa na Kampuni ya MCK ambayo inayojihusisha na masuala ya Uchimbaji wa Madini na Uinjinia ambayo pia ipo chini ya Katumbi.

Pia Mazembe ni kampuni ambayo ina wanashea mbalimbali wenye mchango chini ya mwenyekiti ambaye ni Katumbi. BAJETI Bajeti ya Simba kwa sasa inapaa kutokana na wingi wa mastaa ambao wanavuta mkwanja mrefu klabuni hapo.

Chini ya Mo bajeti ya Simba kwa sasa ni bilioni 2 lakini mwenyewe anataka ipae hadi iguse bilioni 5 ambapo wataweza kushindana na timu kubwa Afrika.

Katumbi alivyoanza kuwekeza Mazembe alianza na bajeti ya Sh.Bil 8.1 badae akaongeza ikafikia Sh. Bil 11.6. Hapo ndipo alipokuwa akinunua mastaa kama kina Mbwana Samatta, Stopila Sunzu na wengine kibao wa Afrika ambao walifanya timu hiyo kuogopwa zaidi.

Kuanzia mwaka 2017, bajeti ya Mazembe ni Sh. Bil 23.2 ambayo inaelezewa kuwa kubwa zaidi katika ukanda wa Afrika Mashariki na Kati.

Hiyo ndiyo jeuri inayowafanya wawe na nguvu ya kuajiri mtu yoyote na kujiendesha kisayansi. Ripoti za hivi karibuni zinasema kwamba Katumbi baada ya kufanya tathmini ya kina ameamua kupunguza mastaa wengi wa nje na kuwekeza kwa wachezaji wengi wa ndani kwa masilahi ya Taifa.

“Hatujapunguza bajeti yetu, tulichofanya ni kuwekeza kwa wachezaji wa ndani wazuri ambao kwenye miaka ya hivi karibuni wamekuwa wakifanya vizuri kuliko hata wageni, kwa kufanya hivyo tutaisaidia pia timu ya taifa na kukuza akademi ya Katumbi,” ilisema taarifa ya Mazembe ikikanusha habari zilizokuwa zimeenea kwenye mitandao kwamba wamepunguza matumizi.

Katika kikosi cha Mazembe bado wapo kina Jean Kimwaki, Joel Kasusula, Tresor Mputu, Miche Mika, Chico Ushindi, Nathan Shinkala na Rainford Kalaba.

Post a Comment

0 Comments