MANCHESTER United ipo katika wakati mgumu kwelikweli, habari ni kuwa timu hiyo haijafunga bao la kawaida kwa muda wa saa nane na dakika 47. Kumbuka kuwa mara ya mwisho kwa United kupoteza mechi saba kati ya tisa katika michuano yote ilikuwa mwaka 1962.
Takwimu za sasa zinaonyesha kuwa, kiungo mkabaji Scott McTominay ndiye mchezaji wa mwisho wa Man Utd kufunga bao la kawaida katika mechi dhidi ya Wolves, Aprili 2, mwaka huu.
Kipigo cha mabao 2-0 ambacho United inayonolewa na Ole Gunnar Solskjaer ilikipata kutoka kwa Man City kimekamilisha takwimu hizo za ukame wa mabao nje ya mabao ya penalti.
Paul Pogba alifunga mabao mawili ya penalti na pia alikuwa wa mwisho kufunga bao katika mechi dhidi ya West Ham, Aprili 13, tangu hapo hakuna mwingine aliyefunga. Pia timu hiyo hajamaliza bila kuruhusu wavu wake kutikiswa katika mechi 12 zilizopita za michuano yote, ni mara ya kwanza kutokea tangu 1971.
Kingine kinachoonyesha hali siyo nzuri ni kitendo cha kocha wa Man City, Pep Guardiola kuwa wa kwanza kuifunga United mechi tatu mfululizo kila anapotua kwenye Uwanja wa Old Trafford unaomilikiwa na United
0 Comments