Windows

Liverpool yaibomoa Huddersfield na kukamata tena usukani

Liverpool kwa mara nyingine wamewawekea mbinyo Manchester City baada ya kurejea kileleni wa ligi kwa ushindi mnono dhidi ya Huddersfield uwanjani Anfield Ijumaa usiku. Vijana hao wa kocha Jurgen Klopp sasa wako kileleni na mwanya wa pointi mbili mbele ya mabingwa watetezi, ambao wana mechi moja ya ziada. Bao la Naby Keita katika sekunde ya 15 liliwafungulia wenyeji lango la mafuriko.

Sadio Mane aliongeza la pili kabla ya Mo Salah kufunga bao la tatu kwa kumvisha kanzu kipa Jonas Lossl na kufanya mambo kuwa 3 – 0 katika kipindi cha mapumziko.

Katika kipindi cha pili, Liverpool waliendeleza mashambulizi yao na Mane akatia kimiani bao la nne na lake la pili kupitia kichwa na kujiunga na kundi la wafungaji wanaoongoza kwenye ligi msimu huu wenye mabao 20 katika ligi ya Premier.

Salah hata hivyo alirejea tena kileleni mwa orodha hiyo kwa kufunga bao la tano la Liverpool na kufikisha idadi ya mabao 21.

Hakuna timu ambayo ishawahi kupata pointi 91 na ikakosa kushinda taji.

Manchester City wanaweza kukamata tena usukani kama watashinda mechi yao ya ziada dhidi ya Burnley Jumapili. Baada ya hapo, timu zote zina mechi mbili za kucheza kabla ya msimu kumalizika.


Post a Comment

0 Comments