

Straika Ramadhani Kapera si Yanga tu, bali hata Simba yenyewe aliwanyoosha Kaitaba kwa kufunga moja ya mabao mawili yaliyowanyamazisha Wekundu wa Msimbazi kwa msimu wa pili mfululizo mjini Bukoba walipowacharaza mabao 2-1.
Sasa unaambiwa mabao mawili dhidi ya Simba na Yanga yamewashtua mabosi wa Msimbazi ambao walikuwa wakikuna vichwa kumvuta straika wa TP Mazembe Mzambia Rainford Kalaba ambaye hata hivyo dau lake limeonekana kuwa kubwa na kumvuta yeye.
Ipo hivi. Mabosi wa Simba wameamua kumleta Kapera jijini Dar es Salaam na kufichwa katika hoteli moja iliyopo Magomeni Mwembechai kabla ya Simba haijasafiri kwenda mjini Morogoro kucheza mechi dhidi ya Mtibwa Sugar.
Hata hivyo, pilikapilika za mechi ya Morogoro, zilifanya Kapera akae hotelini hapo bila kuonana na mabosi wa Msimbazi ambapo jukumu la kumsainisha lilikuwa kwa Ofisa Mtendaji Mkuu wa Simba, Crescentius Magori.
Mwanaspoti inafahamu mbali ya kuwepo mawilisiano ya karibu kati ya Kapera na Magori muda wowote anaweza kujiunga na mabingwa hao kwa ajili ya msimu ujao, japo kocha wa Simba, Patrick Aussems ameonyesha pia kuvutiwa na mshambuliaji mwingine wa mzawa wa Mtibwa Sugar, Salum Kihimbwa ambaye bado ana mkataba na timu yake.Mmoja wa kiongozi wa juu wa Simba alisema wajumbe wa Bodi ya Wakurugenzi wametuliza akili katika kufanya usajili wa msimu huu kulingana na upungufu ulioonekana katika mashindano yote waliyoshiriki msimu uliopita lakini kwa muongozo wa matakwa ya kocha wao Aussems.
“Tulikuwa na mazungumzo ya karibu na Kapera ambaye nadhani anaweza kuwa nasi msimu ujao kama mambo yatakwenda sawa na tutakubaliana masuala ya kimkataba. Kuhusu Kihimbwa naye ni sehemu ya mapendekezo kocha wetu, amekuwa akiwatolea mfano wanaweza kuongeza nguvu katika timu yetu msimu ujao,” alisema kiongozi huyo.
“Katika vikao vya Bodi ya Wakurugenzi na Aussems miongoni mwa wachezaji ambao tumewajadili mpaka wakati huu ni Kapera, Kihimbwa na Francis Kahata ambao wote wamependekezwa na kocha, lakini bado tupo katika soko la usajili tukitafuta wachezaji wengine kwani tunatakiwa kusajili wachezaji wapya wasiopungua wanne,” alisema kiongozi huyo aliyeomba kuhifadhiwa majina yake.
GYAN, KWASI SASA
Katika hatua nyingine mabosi hao wa Simba ili waweze kusajili mchezaji mpya wa kigeni watalazimika kupunguza idadi ya waliokuwa nao, kwani tayari wana majembe 10 na sheria inaelekeza wasizidi idadi hiyo na fasta kuna wachezaji watapigwa panga.
Beki kiraka Asante Kwasi na Nicholas Gyan wapo kwenye hatihati ya kusalia Msimbazi kwa mujibu wa chanzo hicho makini, huku Zana Coulibaly akiwagawa mabosi wa Simba kwa vile Kocha Aussems anamtaka na wao wakitaka apigwe chini kwani hana maajabu.
“Wachezaji hao watatu wapo katika hati hati ya kutokuwa nasi msimu ujao lakini kuhusu Coulibaly kocha Aussems amekuwa anamkingia kifua akitaka aende naye katika maandalizi ya msimu akiamini atarudi akiwa bora ila bodi haijaridhika nalo,” alisema.
“Kuhusu Juuko Murshid bado hatujaelewana naye, hivyo lolote linaweza kutokea dhidi yake kama ilivyokuwa kwa Emmanuel Okwi ambaye ametuomba kwanza akacheze Afcon akiwa mchezaji huru,” alisema kiongozi huyo ambaye aliomba jina lake lisiwekwe wazi kwa sababu za kiusalama.
Mbali na hao pia jina la James Kotei limekuwa nalo likihusishwa katika panga, ingawa mwenyewe ameliambia Mwanaspoti hajui lolote kama ambavyo Gyan naye alivyosema.
Gyan alisema anatarajia kuondoka nchini Jumapili kwenda kwao kwa mapumziko baada ya ligi kuisha, ila anazo ofa moja Marekani na kama mambo yakienda vyema, Simba ndiyo basi tena.
“Hadi sasa sijajua hatma yangu, ila kikubwa ninachoweza kusema sitachukua uamuzi wowote hadi nitakapopata tamko kutoka kwa viongozi wa Simba kama wananihitaji au hawana mpango na mimi kwa msimu ujao,” alisema Gyan.
Naye Kotei alisema; “Bado nipo Dar sijajua nitaondoka lini, kubwa nasubiri kujua hatma yangu Simba niliyoichezea misimu mitatu na misimu yangu miwili ya mwisho nikibeba nao ubingwa wa Ligi Kuu.”
MAGORI HUYU HAPA
Ofisa Mtendaji Mkuu wa Simba, Magori alipoulizwa juu ya suala la usajili wa klabu hiyo, alisema, bado hawajapata ripoti ya mwalimu kuhusiana na nyota anaotaka wasajiliwe na idadi ya wanaopaswa kuongezewa mikataba hivyo hawezi kulizungumzia.
“Mwalimu kafika Dar es Salaam jana (juzi) akitoka Morogoro leo (jana) alipewa muda apumzike nadhani kesho anaweza kukutana na viongozi ili aweze kukabidhi ripoti, hivyo suala hilo la usajili siwezi kuzungumza lolote kwa sasa,” alisema.
Hata hivyo, mapema Magori alinukuliwa na Mwanaspotui akisema kuwa, klabu yao itafanya usajili wa kishindo kulingana na mapendekezo ya benchi lao la ufundi kwa nia ya kufika mbali zaidi ya walipofikia msimu huu ikiwamo kucheza robo fainali ya Ligi ya Mabingwa Afrika.
Magori alisema wachezaji watakaosajiliwa kwa ajili ya msimu ujao watakuwa bora na wenye uwezo ili kukiongezea nguvu kikosi cha Wekundu wa Msimbazi ili kiweze kutamba zaidi ndani na nje ya nchi.




0 Comments