Windows

Gor Mahia waanza kunusa tena ubingwa wa ligi

Vigogo Gor Mahia walitoka nyuma na kuwalaza Nzoia Sugar 2-1 katika mechi ya kiporo ya ligi kuu nchini Kenya – KPL iliyosakatwa ugani Moi mjini, Kisumu Jumatatu.

Gor ambao ni viongozi wa ligi walienda kwenye mechi hiyo wakisaka ushindi ambao ungewawezesha kutanua uongozi wao katika jedwali ya KPL hadi pointi 41 wakiwa na mechi moja mkononi.

Na hili nyusoni mwao, mambo hayakuwaanzia vyema kwani mshambulizi wa zamani wa timu ya Nairobi Stima na Thika United, Hansel Ochieng aliwapa Nzoia uongozi katika dakika ya pili kupitia mkwaju wa penalti.

Dakika tano baadaye, nahodha wa zamani wa Harambee Stars, Dennis Oliech alimpa kiungo wa Burundi Francis Mustafa pasi Safi naye akaisawazishia Gor Mahia.

Timu zote mbili zilitengeneza nafasi nyingi za kufunga mabao kipindi cha pili ila mastraika wao walisuasua na kukosa kumakinika mbele ya lango swala ambalo liliwagharimu hasa wageni Nzoia kwani dakika tatu kabla ya kipienga cha mwisho kupulizwa, beki Geoffrey Ochieng aliifungia Kogalo bao la pili kwa kichwa baada ya kuandaliwa pasi murwa na George Blackberry Odhiambo.

Ushindi huo uliusaidia Gor Mahia kuzidisha uongozi wao kwa alama tano. Sasa hivi mabingwa hao mara 17 wanaongoza jedwali hilo la timu 18 kwa alama 41, tano zaidi ya nambari Sofapaka japo wana mechi moja mkononi baina ya Sony Sugar wanaochuana nao Alhamisi hii.

Baadaye watarejea jijini Nairobi kujiandaa kuvaana na RS Berkane ya Morocco kwenye mkumbo wa kwanza wa robo fainali ya kombe la Shirikisho Afrika siku ya Jumapili katika uchanjaa wa Kasarani.

Ikumbukwe Gor waliwanyuka Kariobangi Sharks 2-1 siku ya Jumamosi mjini Kisumu ushindi wa leo ukiwa wa pili chini ya masaa 72 katika kaunti hiyo yenye joto kali. Je, Gor itakusanya jumla ya pointi tisa siku ya Alhamisi dhidi ya Sony?


Post a Comment

0 Comments