Windows

DIAMOND APEWA MTIHANI HUU MZITO NA BABA YAKE


MOJA kati ya matukio yaliyotikisa ndani ya wiki iliyopita ni lile la kupatana kwa mwanamuziki Nasibu Abdul ‘Diamond Platnumz’ na baba yake Abdul Jumaa ambapo baada ya kupatana huko, msanii huyo amepewa mtihani mzito ambao akiufaulu, itaaminika kuwa kilichofanyika siyo kiini macho.

Kupatana kwa wawili hao kumekuja baada ya figisu za muda mrefu ambazo zilihitimishwa Jumanne iliyopita ndani ya Studio za Wasafi TV ambapo waliamua kuzika tofauti zao na kufungua ukurasa upya.

Hatua hiyo iliwafurahisha wengi ambao hawakuwa wakivutiwa na umbali uliokuwepo kati ya baba na mwanaye huyo hivyo pongezi nyingi zikamiminika kwa Diamond.

Mbali na pongezi hizo, ndugu na mashabiki wa staa huyo walimpa mtihani mzito na kusema akiufaulu wataamini kilichotokea ni kweli na siyo kiki kama baadhi wanavyodhani. 

Akizungumza na Ijumaa Wikienda, mmoja wa ndugu wa baba Diamond aliyejitambulisha kwa jina la Swedi Juma alisema, wamefurahishwa na hatua aliyofikia ndugu yao na mwanaye lakini wataamini kama kweli wamezika tofauti zao endapo atamfanyia mambo muhimu kama mzazi.

“Nisiwe mnafiki, kuna wakati nilikuwa namchukia sana Diamond kwa alichokuwa akimfanyia baba yake lakini kwa hili lililotokea, nimefarijika sana. Ila nampa mtihani, akiufaulu sisi ndugu zake na hata mashabiki zake tutaamini kwamba kweli wako sawa.

“Cha kwanza, yule mzee anaumwa miguu na amekuwa akilalamika kwamba hana pesa za matibabu. Diamond ampeleke India, amtibu tatizo lake hilo, hapo tutaamini kweli amerudisha mapenzi kwake.

“Lingine, ile nyumba anayoishi mzee Abdul kule Magomeni haina hadhi ya kuwa ya baba wa staa mkubwa, wala asimjengee nyumba mpya, ileile tu aikarabati kama alivyoifanya ile nyumba yao ya kule Tandale.

“Cha mwisho, sidhani kama Diamond anashindwa kumpa usafiri baba yake. Amnunulie kigari cha kufanyia mizunguko ya hapa na pale. Mimi nakuambia endapo atafanya hayo, kisha akawa anamtoa kishikaji pesa za matumizi, sisi ndugu tutaamini kwamba upendo umerejea na Mungu atambariki zaidi ya hicho alichonacho sasa,” alisema ndugu huyo. Mbali na huyo, wadau wengi kwenye mitandao ya kijamii wameonesha kufurahishwa na kupatana kwa wawili hao lakini nao wakapita mulemule kwamba, isiishie kwenye TV tu bali Diamond sasa amfanyie baba yake anayostahili ambayo ameyakosa kwa muda mrefu.

“Ni tukio la kihistoria na mimi naamini sasa hata maisha ya Mzee Abdul yatabadilika. Ilikuwa wakati mwingine ngumu kuamini kwamba yule ni baba wa staa lakini kupatana kwao huko sasa kuendane na mabadiliko,” aliandika Instagram mtu aliyejiita Shebby.


Mwingine aliyejiita Wakusaundi aliandika: “Wengi wanataka kuona what next (nini kitafuata), je, maisha ya baba D yatabadilika? Yakibaki palepale Diamond atakuwa amefeli mtihani ambao naamini wengi wanasubiria majibu yake. Kikubwa sasa hiviamtunze na amfanye aonekane ni baba wa staa.” Mwandishi wetu alifanya jitihada za kumtafuta Diamond ili kujua kama yuko tayari kumfanyia baba yake yale ambayo wengi wanatarajia lakini simu yake haikuwa hewani.

Hata hivyo, siku chache kabla ya msanii huyo kupatana na baba yake alisema kuwa, alikuwa kwenye mchakato wa kumpeleka India kwa ajili ya matibabu lakini akashangaa kuona yanaibuka manenomaneno yaliyomkatisha tamaa. Kwa upande wake Baba Diamond aliliambia Ijumaa Wikienda kuwa, amefurahishwa na hatua waliyofikia na mwanaye na kwamba anatarajia mabadiliko kwenye maisha yake.

Post a Comment

0 Comments