KOCHA Mkuu wa Yanga, Mwinyi Zahera, amesema anataka kabla ya Ligi Kuu Bara kumalizika, wachezaji wote anaowahitaji wawe wameshasaini mikataba mipya ya kubaki kuendelea kuichezea timu hiyo.
Kocha huyo alitoa kauli hiyo mara baada ya kupata taarifa za baadhi ya wachezaji kumaliza mikataba yao huku wengine wakidai kuwa na mpango wa kuihama timu hiyo msimu ujao.
Kati ya wachezaji ambao mikataba yao inamalizika ni Ibrahim Ajibu, Papy Tshishimbi, Gadiel Michael, Ramadhani Kabwili, Abdallah Shaibu ‘Ninja’ na Amissi Tambwe.
Zahera alisema hatakubali kumuachia mchezaji yeyote atakayemhitaji katika kikosi chake msimu ujao. Zahera alisema anafanya kupunguza presha inayotokea katika kipindi cha usajili ambacho wachezaji wengi wanatishia kuondoka na kusababisha dau la usajili kuongezeka.
“Wengi walikuwa hawajui malengo ya kuchangisha fedha hizi ambazo mimi ndiyo nazisimamia mwenyewe. Ninataka fedha hizo zinazotokana na michango ya mashabiki kutumika kwa ajili usajili wa msimu ujao wa ligi na kama unavyofahamu wachezaji wote nimewakuta isipokuwa Boban pekee.
“Hivyo, ni lazima nisajili wachezaji wangu wale ninaowahitaji katika msimu wangu mpya kabisa na wale waliopo hivi sasa ambao mikataba yao inamalizika kwa kuwaongezea mipya.
“Uzuri ni kuwa tayari nimemaliza kazi yangu hiyo ya usajili kwa wale wachezaji ninaowahitaji waongezewe mikataba, sitakuwa na kibarua kigumu, tayari nimeshawaambia viongozi wangu ninataka kabla ya ligi kumalizika wachezaji wote ninaowahitaji wawe tayari wamesaini mikataba,” alisema Zahera.
0 Comments