LIPULI kuna hali mbaya. Wachezaji wamegoma kufanya mazoezi kisa ni mishahara na fedha za usajili. Kwa mujibu wa taarifa ambazo imezipata Spoti Xtra, wachezaji hao wanadai mishahara ya miezi mitatu ambayo waliahidiwa kulipwa na viongozi wa timu hiyo baada ya mchezo wa Ligi Kuu Bara na Simba.
“Hatutaki kuonana wasaliti wachezaji, wote kwa pamoja tumekubaliana kutofanya mazoezi.
“Kwa sababu tunaona kama ubabaishaji unaofanywa na viongozi wetu mwenyewe walituahidi kutulipa mishahara yetu ya miezi mitatu na fedha za usajili tunazodai ambazo hadi leo hatujalipwa tulizoahidiwa kulipwa baada ya mechi ya Simba,” alidokeza mchezaji mmoja na kuongeza.
“Cha kushangaza baada ya mechi hiyo tukiwa safarini tukirudi Iringa tukitokea Bukoba kucheza na Kagera Sugar wakatuingizia mshahara wa mwezi mmoja ambao ni nusu tena, kiukweli tumechukizwa na kitendo hicho.” Alipoulizwa kocha wa timu hiyo, Selemani Matola kuzungumzia hilo, alisema kuwa
“Nikiri kuwepo kwa hali hiyo katika timu, wachezaji wamegoma kufanya mazoezi sababu ikiwa ni madai yao ya mishahara na fedha zako za usajili wanazodai. “Waliahidiwa na viongozi kuwalipa madai yao ambayo hadi leo hawajalipwa, binafsi kama kocha hali hii inanivurugia mipango yangu katika kuiandaa timu.”
CHANZO: SPOTI XTRA
0 Comments