DAR ES SALAAM: FUNZO kubwa! Ndiyo kauli iliyosikika katika vinywa vya wengi, kuelezea vifo vya Mkurugenzi wa Vipindi na Uzalishaji wa Clouds Media Group, Ruge Mutahaba na Mtangazaji wa Clouds FM, Ephrahim Kibonde vilivyotokea ndani ya muda mfupi.
Ruge alifariki dunia Februari 26, mwaka huu alipokuwa nchini Afrika Kusini kwa matibabu huku Kibonde akifariki alfajiri ya Machi 7, saa chache baada ya kumaliza zoezi la mazishi ya Ruge.
KWA NINI FUNZO?
Waombolezaji wengi waliozungumza na Ijumaa Wikienda, walieleza namna misiba hii ilivyoacha fundisho kubwa kwa jamii katika vipindi tofauti. Kuna ambao walieleza namna ambavyo kifo cha Kibonde kimegusa mamilioni ya Watanzania kutokana na jinsi alivyoongoza kama MC wa msiba wa Ruge kuanzia jijini Dar hadi Bukoba alikokwenda kupumzishwa Ruge katika makazi yake ya milele.
“Hii ni zaidi ya somo kwetu sisi tuliobaki. Kwa waliomuona Kibonde pale katika Viwanja vya Karimjee, hakuna hata mmoja aliyedhani kwamba naye anaweza kudondoka leo au kesho. Kila mtu alimuona Kibonde yupo safi na mwenye afya njema hata kusimamia shughuli nzito kama ile,” alisema msanii wa Bongo Movies, Kulwa Kikuba ‘Dude’.
MANENO YA KIBONDE
Mbali na kumuona tu Kibonde ni mzima wa afya siku hiyo, maneno aliyoyazungumza siku ya kuaga mwili wa Ruge katika viwanja hivyo, ndiyo yamekuwa chachu ya watu kujitafakari na kila mmoja kueleza jinsi ambavyo ameguswa na kujifunza sana katika vifo hivi.
“Kwa kweli yale maneno ya Kibonde aliyoyasema kwamba mtu unaweza kufa leo, kama si leo kesho na kama si kesho basi kesho kutwa yamekuwa zaidi ya somo kwangu. Kwa umri wangu huu na jinsi ninavyojifunza kila siku nafahamu kwamba kifo ni lazima lakini kwa yale maneno, nimeuona uhalisia wake.
“Kitendo cha yeye kusema kama si kesho basi ni kesho kutwa na kweli ameondoka, ile imetufanya hata sisi wasanii tujitafakari upya. Tunapaswa kumrudia Muumba wetu na kuishi katika misingi ya sala,” alisema muigizaji Blandina Chagula ‘Johari’.
KWA UPANDE WA RUGE
Kifo cha Kibonde kimeonekana kuibua upya kifo cha Ruge na kuwafanya watu wengi hususan mitandaoni wamkumbuke na kuyajadili yale mema ambayo aliyafanya akiwa hapa duniani na watu wengi kuyabaini baada ya kuondoka.
Mmoja wa waombolezaji aliyejitambulihsa kwa jina la Juma Kihoi aliyekuwa msibani, nyumbani kwa wazazi wa Kibonde, Mbezi-Africana, alisema kifo cha Kibonde kimemfanya arudi nyuma kimazo na kumkumbuka Ruge na kuona hata yeye ndivyo anavyopaswa kuishi.
“Niwe mkweli nilikuwa simfuatilii sana Ruge lakini kutokana na historia na ukubwa wa msiba wake nilioushuhudia na jinsi shuhuda mbalimbali zilivyotolewa wakati wa kuaga, niligundua Ruge ametuachia somo kubwa sana.
“Ruge ametupa darasa la maisha kwamba hapa duniani sisi si kitu hivyo tunapaswa kufanya kila tuwezavyo kuhakikisha tunawatendea mema watu wanaotuzunguka. Ruge aligusa maisha ya mtu mmojammoja, hakuwa mchoyo. Aligawa mawazo na alikuwa tayari hata kukopa ili amsaidie mwenye shida.”
MANARA NAYE AGUSWA
Msemaji wa Klabu ya Simba, Haji Marana naye alionesha kuguswa na vifo hivi moja kwa moja na kuandika ujumbe kwenye ukurasa wake wa Instagram kwamba ameamua kuwa mtu wa kuswali.
“Mtanisamehe sana, maisha ya kibitozi yananitisha maana kifo hakiangalii wewe Msemaji wa Simba wala unajua sana kuimba! Kifo hakina hodi na hakijali account zako za benki na kina desturi ya kuzunguka. Now kipo Clouds, hujui kitahamia wapi! Ahhh sasa hivi ni swala hadi malaika waseme yes,” aliandika Manara.
Mwili wa Kibonde ulizikwa juzi katika Makaburi ya Kinondoni jijini Dar ambapo msiba huo ulihudhuriwa na umati mkubwa ulioongozwa na Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam, Paul Makonda pamoja na viongozi wengine wa Serikali akiwemo Waziri wa Maliasili na Utalii, Dk Hamisi Kingwangalla. Pia alikuwepo Rais mstaafu wa Awamu ya Nne, Dk Jakaya Kikwete na mkewe Salma.
MKEWE ALITANGULIA
Ikumbukwe pia, Kibonde amefariki siku 240 baada ya mkewe Sara kufariki Julai 10, mwaka jana.
WATOTO
Kibonde ameacha watoto watatu; Junior, Hilda na Illaria. Mungu ailaze roho yake mahali pema peponi-amina!
Stori: Erick Evarist na Richard Bukos, Ijumaa Wikienda
0 Comments