Windows

TRAFIKI ANUSURIKA KUFA KWA KUGONGWA NA BAJAJI KAHAMA




Askari polisi kitengo cha usalama barabarani Kahama Mjini WP. 10492 PC Jenipher amenusurika kufa baada ya kugongwa akiwa kazini katika barabara ya Kahama kwenda Kiinza Tabora.



Kwa mujibu wa taarifa kwa vyombo vya habari kutoka kwa Kamanda wa polisi mkoa wa Shinyanga ACP Richard Abwao tukio hilo limetokea leo Jumanne Machi 12,2019 majira ya
saa tatu asubuhi katika eneo la Mhungula Mashineni barabara ya Kahama kwenda Kiinza Tabora, kata ya Mhungula,Tarafa ya Kahama Mjini, wilaya ya Kahama na Mkoa shinyanga wakati askari huyo akiendelea kutekeleza majukumu yake.


Amesema pikipiki (bajaji ya mizigo) yenye namba za usajili MC 649 BVE WANHOO, mali ya mtu asiyejulikana kwa jina, ikiendeshwa na dereva asiyejulikana kwa jina, kabila wala umri ikitokea Mjini Kahama kwenda Kiinza ilimgonga askari polisi huyo wa kitengo cha usalama barabarani na kusababisha majeraha katika sehemu mbalimbali za mwili wake.


“Askari polisi amepata majeraha kichwani na usoni na michubuko kwenye mikono yote miwili, pia kusababisha majeraha ya miguu yote miwili kwa abiria aliyekuwa kwenye bajaji hiyo Andrew Michael (29) mkazi wa Zongomela Kahama”,ameeleza Kamanda Abwao.




“Chanzo cha ajali hiyo ni mwendokasi wa dereva wa bajaji hiyo, askari huyo amelazwa hospitali ya wilaya ya Kahama na hali yake inaendelea vizuri kwa sasa. Dereva wa bajaji hiyo amekimbia baada ya ajali, na juhudi za kumkamata zinaendelea, bajaji hiyo ipo kituo cha polisi Kahama”,ameongeza Kamanda Abwao.

Post a Comment

0 Comments