Kikosi cha Simba kimerejea jijini Dar kikitokea Algeria kilipokuwa kuivaa JS Saoura.
Akitua kwenye Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Julius Nyerere (JNIA) Jana, Kocha Mkuu wa Simba, Patrick Aussems ametamba kuwa kama wamewafunga Al Ahly na JS Saura basi As Vita nao wanakufa nyumbani.
Simba jana ilirejea jijini Dar es Salaam ilipokwenda kucheza na JS Saoura ya Algeria katika hatua ya makundi ya Ligi ya Mabingwa Afrika ambako walifungwa mabao 2-0.
Timu hiyo, Jumamosi hii saa moja kamili inatarajiwa kushuka kwenye Uwanja wa Taifa jijini Dar es Salaam kuvaana na Vita mchezo unaotarajiwa kujaa upinzani mkubwa.
Akizungumza na SALEHJEMBE Mara baada ya kutua uwanja huo wa ndege, Aussems alisema kuwa tayari alishaanza maandalizi ya mchezo huo tangu akiwa Algeria na kikubwa anahitaji ushindi wowote ili kufanikisha malengo yao ya kwenda hatua ya robo fainali.
Aliongeza kuwa, anawafahamu vizuri Vita ambao alicheza nao katika mchezo wa awali uliochezwa Congo Kinshasa, hivyo hana hofu baada ya kuyafanyia marekebisho baadhi ya makosa.
"Mchezo wetu na Saoura ulikuwa mgumu kwa upande wetu kutokana ukubwa wa safari yenyewe ambao ulisababisha wachezaji kuchoka.
"Tayari nimewaambia wachezaji wangu kusahau matokeo ya mechi na Saoura na badala yake kuelekeza nguvu katika mchezo na Vita.
" Tunaamini mechi haitakuwa nyepesi kwetu, lakini kwa maandalizi niliyoyafanya na sapoti ya mashabiki ninaamini hatutapoteza mchezo huu, alisema na kuongeza.
"Leo baada ya timu kurejea moja kwa moja tunaelekea kambini kwa ajili ya maandalizi ya mchezo huu.
0 Comments