Windows

JUMAMOSI, SIMBA WANA KILA SABABU KUIKATAA BAHATI MBAYA







NA SALEH ALLY
BAADA ya kipigo cha mabao 2-0 walichokipata Simba kutoka kwa JS Saoura, kundi lao limekuwa huru au wazi kwa timu yoyote kuweza kufuzu katika hatua ya robo fainali ya Ligi ya Mabingwa Afrika.

Uwazi huo unatokana na kwamba kati ya timu zote nne zilizo katika kundi hilo zina nafasi ya kufuzu kwa usawa kabisa.

Mechi za mwisho ziko hivi; Simba itakuwa nyumbani dhidi ya AS Vita ambayo mechi ya kwanza nyumbani ilishinda kwa mabao 5-0. Al Ahly itakuwa nyumbani Misri kuwasubiri Saoura ambao dhidi yao wakiwa nyumbani walipata sare ya bao 1-1.

Simba wana nafasi ya kufuzu kwa kuwa sasa wanashika mkia wakiwa na pointi sita na kama watashinda dhidi ya AS Vita, watafikisha tisa ambazo Vita hawawezi kuzifikia na kama Saoura atashinda watakuwa na 11 na Ahly atabaki na saba.

Kama Saoura atapoteza maana yake atabaki na nane ambazo zitakuwa zimepitwa na Simba. Kama itatokea kuwa sare, basi Saoura atakuwa na tisa na Ahly atafikisha nane, bado kama Simba atakuwa ameshinda, atafuzu.
Maana yake iko hivi, hakuna mjadala na Simba wanachotakiwa ni kushinda mechi hiyo ya mwisho jijini Dar es Salaam.

Kama unakumbuka, mkakati wa Simba ulikuwa ni kushinda mechi zote tatu za nyumbani, angalau kupata hata sare moja ili kuwa na poini 10.

Mpango wa kwanza kama plani, unaonekana kuwa umekwama kwa kuwa Simba wamepoteza mechi zote tatu za ugenini dhidi ya Vita, Ahly na Saoura.


Sasa karata iko kwao kwa upande wa nyumbani, mechi ambayo haitakuwa lelemama hata kidogo kwa kuwa Vita watakuwa pia wanataka kufuzu na wanajua kuwang’oa Simba halitakuwa jambo rahisi, hivyo watatua Dar es Salaam, wakiwa wamejiandaa hasa.

Hakika ni kazi ngumu lakini kufuzu kazi inayoonekana si ya mchezo ndiyo kunaonyesha thamani yako na Simba ndicho watatakiwa kukifanya ili kubadilisha mambo.
Unapokutana na wakati mgumu kama huo unakuwa ni wakati mzuri wa kupima ukubwa au ubora wako wa kushughulika na mambo magumu uko katika kiwango kipi.
Simba wanapaswa kushinda mechi hiyo bila ya kuonyesha wanakumbuka au hofu ya kufungwa mabao 5-0 dhidi Vita kwenye mechi yao ya kwanza.

Kundi D limeonyesha rekodi za nyuma hazina msaada, tumeona Ahly walioifunga Simba mabao 5-0 na Vita mabao 2-0, imepoteza mechi zake zote za ugenini dhidi ya timu hizo.

Saoura alifungwa 3-0 na Simba mechi ya ufunguzi, naye ameshinda 2-0 nyumbani. Maana yake kila timu ina uwezo wa kushinda bila ya kujali mechi yao ya nyuma ilikuwaje.

Simba pia inapaswa kuingiza kumbukumbu zinazoonyesha katika kundi lao, hakuna timu imefungwa nyumbani, maana yake kila mmoja kulinda pointi za nyumbani kwani waliopoteza ni Saoura waliotoka sare na Al Ahly na Vita aliyetoka sare na Saoura.

Hivyo, Simba wana nafasi kubwa ya kutengeneza kile kinachoeleweka na kuonyesha ukomavu kwa kushinda mechi hiyo.

Ni kitu kimoja tu kinatakiwa. Simba kushinda mechi hiyo japo Vita ni timu bora lakini wana kila sababu na kuthibitisha kuwa wana uwezo wa kushinda.

Kuanzia maandalizi, wachezaji kuonyesha ukomavu na kocha kukipanga kikosi vema. Mwisho kinachotakiwa ni mapambano yenye tahadhari na mwisho ni matokeo chanya. Simba wasitishwe wala kuaminishwa tofauti, ushindi ndicho kitu kinachotakiwa na inawezekana. 



Post a Comment

0 Comments