Windows

SHABIKI WA SIMBA KUTOKA KAGERA ASHINDA MILIONI 84 ZA M-Bet



SHABIKI wa Simba kutoka mkoani Kagera, Semistocles Mkiza, ameshinda Sh 84,814,160 kupitia Kampuni ya Michezo ya Kubashiri ya M-Bet.

Mkiza ambaye anajishughulisha na uvuvi wa dagaa katika Ziwa Victoria, ameshinda kiasi hicho katika droo ya nne iliyochezeshwa Machi 24, mwaka huu.

Akimtangaza mshindi mbele ya waandishi wa habari jijini Dar es Salaam, Msemaji wa M-Bet, David Malley, amesema Mkiza ni miongoni mwa washindi wao watatu waliobashiri mechi 11 kwa usahihi kati ya mechi 12 za Parfect 12.

"Mshindi wetu wa droo ya nne iliyochezeshwa Machi 24 ni ndugu Semistocles Mkiza. Yeye ni miongoni mwa washindi watatu wa jackpot yetu ya Perfect 12 ambapo alipatia mechi 11.

"Katika Perfect 12, kuna washindi wa aina nne, wanaopatia mechi zote 12, wengine 11, wapo wa mechi 10 na 9 ambapo wote hao kuna bonus tumewapatia, lakini kwenye droo yetu huyu ndiye mshindi.

"Katika fedha hizi kuna asilimia 20 tunazipeleka TRA ambapo ni zaidi ya Sh milioni 16, hivyo mtaona ni namna gani tunavyohusika kuhakikisha tunatimiza agizo la ulipaji kodi kama serikali inavyoagiza," amesema Malley.

Akizungumzia ushindi wake, Mkiza amesema: "Kwanza namshukuru Mungu kwa ushindi huu, nimeanza siku nyingi kubeti na hii ni mara yangu ya kwanza kushinda.

"Hizi fedha nitazitumia katika suala la elimu kwa wanangu ambao ninao sita, lakini pia katika biashara yangu ya dagaa. Pia nitatafuta njia nyingine ya biashara.

"Mimi ni shabiki mkubwa wa Simba, najua wanacheza na TP Mazembe Aprili 6 hapa jijini Dar, hivyo katika hizi fedha, kiasi kidogo nitakitumia kwa ajili ya kutoka Kagera kuja Dar kuisapoti timu yangu ishinde."


Katika hatua nyingine, Mkiza amesema tangu azaliwe na sasa ana miaka 41, hakuwahi kufika Dar, anawashukuru M-Bet kwa kumfikisha Dar kwa mara ya kwanza kwani bila ya kushinda na M-Bet alikuwa hajui lini atafika Dar.

Post a Comment

0 Comments