WAZIRI wa Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo, Dk Harrison Mwakyembe, amesema anajua kwa nini wanariadha wengi hapa nchini wanashindwa kufurukuta kwenye mashindano mbalimbali wanayoshiriki.
Mwakyembe aliyasema hayo hivi karibuni akiwa mjini Moshi mkoani Kilimanjaro alipokuwa mgeni rasmi wa mashindano za Kilimanjaro Marathon, ambapo wanariadha kutoka Kenya walifanya vizuri, huku Watanzania wengi wakianguka.
Kauli ya Mwakyembe ya wapi wanariadha wa Tanzania wanakwama, ilikuja baada ya matokeo ya mbio za km 42 (Full Marathon) mshindi wa kwanza hadi wa sita wakitokea nchini Kenya na Mtanzania Stephano Huche akishika nafasi ya saba huku wa nane hadi wa 10 wakiwa ni Wakenya.
“Bado sijaridhika na matokeo ya wanariadha wa Tanzania kwenye mashindano yanayotukutanisha na nchi pinzani, matokeo ya Kili Marathon naweza kusema yanafanana na huu mfano wa kwenye miti hakuna wajenzi.
“Kwa matokeo haya ninam samehe Rais wa Shirikisho la Riadha Tanzania (RT), Anthony Mtaka, ukweli ni kwamba hatuna mpangilio mzuri wa michezo yetu na mimi hili nalichukua kama lawama kwa wizara yangu, tunafanya mambo mengi mno kwa wakati mmoja.
“Sasa hivi kuna mashindano ya Majeshi (BAMMATA) yanaendelea jijini Dar es Salaam, na mbio hizi za Kili km 24 na km12 ndizo zinakimbiwa, sasa hatuwezi kwenda kwa vurugu hivi, hata kama tuna wanariadha wazuri hatutafika, kwa hili nitaitisha kikao, lazima tuwe na kalenda yenye mpangilio mzuri,” alisema.
0 Comments