KOCHA Ole Gunnar Solskjaer ameahidi kupambana kwa ajili ya kurejesha sifa ya timu yake ya Manchester United katika kupigania mataji.
Kocha huyo ambaye klabu yake inamiliki Uwanja wa Old Trafford alitangazwa kuwa kocha rasmi wa timu hiyo kwa mkataba wa miaka mitatu baada ya kuwa wa muda kwa miezi mitatu, ameahidi kuwa hilo la ubingwa ndilo ambalo analifikiria.
Mkataba wake ni wa pauni milioni 7 kwa mwaka, ukiwa umechagizwa na kurejesha ushindi kikosini hapo baada ya kuwa na msimu mbovu chini ya Kocha Jose Mourinho ambaye alifukuzwa Desemba, mwaka jana.
“Ubingwa wa Premier League ndilo tunalowaza kwa sasa, kunyanyua taji ndilo jambo muhimu kwetu, tunataka kurejesha hali hiyo japokuwa siyo kazi nyepesi.
“Nataka nikiondoka niwe nimeshinda mataji, likiwemo la Premier League, ikiwa hivyo nitakuwa najivunia uwepo wangu klabuni hapa,” alisema Ole na kuongeza: “Nina furaha na ni mtu ninayepambana, nataka siku nikiondoka niwe na heshima.”
Wakati huohuo, United imeamua kutoa zawadi ya fedha kwa klabu ya zamani ya kocha huyo, Molde pauni 500,000 (Sh bil 1.5) kama sehemu ya kushukuru kwa kumruhusu Solskjaer kuondoka.
Solskjaer pia amethibitisha kuwa msaidizi wake, Mike Phelan naye ataendelea kuwa naye klabuni hapo japokuwa atalazimika kumalizana na waajiri wake wa zamani waliomtoa kwa muda, Central Coast Mariners ya Australia.
0 Comments