KLAUS Kindoki jana alivua jezi yake huku akipiga kifua chake mara kadhaa akiwaambia mashabiki wa Simba; “Leteni fyokofyoko tena” Kipa huyo raia wa DR Congo ambaye mashabiki wa Simba na Alliance jana walikuwa wakimkejeli kwa madai kuwa hana uwezo, ndiye aliyeibuka shujaa wa mchezo kwa kupangua penalti muhimu zilizoipeleka Yanga nusu fainali ya Kombe la Shirikisho.
Baada ya kutoka sare ya bao 1-1 ndani ya dakika 90, kanuni ziliamuru kwenda kwenye penalti ambako ndiko Kindoki alipoibuka shujaa na kuibuka shangwe ndani ya CCM Kirumba.
Mashabiki wa Yanga jana kwenye mitandao ya kijamii walimuomba radhi pia Kindoki kwa kumkejeli na kutomuamini kipindi cha nyuma.
Katika kipindi cha kwanza mchezo huo ulionekana kuchangamka kutokana na mashambulizi ya hapa na pale huku ikiwatumia Yanga dakika 38 kupata bao lililofungwa nje ya kumi na nane na Heritier Makambo akipokea pasi ya Pius Buswita.
Alliance wakatulia na kuanza kupiga mipira mirefu ambayo kipindi cha pili dakika ya 62, Joseph James akafunga kwa kichwa mpira uliomshinda Kindoki na kuibuka shangwe kwa mashabiki wa Simba na Alliance.
Vijana hao wa Mwanza wakafanya mabadiliko kwa kumtoa Paul Maona wakamuingiza Hussein Javu, wakamtoa pia Michael Chinedu wakamuingiza Samir Vicent. Yanga nao wakamtoa Amissi Tambwe wakamuingiza Haruna Moshi. Badae wakawatoa Buswita na Feitoto wakaingia Deus Kaseke na Thabaan Kamusoko.
Mabadiliko hayo yalionekana kuuchangamsha mchezo huo lakini matokeo yakabaki sare mpaka timu hizo zilipokwenda kwenye penalti. Kelvin Yondani alikosa penalti ya kwanza ya Yanga huku Mrisho Ngassa pia akimpasia kipa. Yanga waliopata penalti ni Paul Godfrey, Kamusoko, Boban na Kaseke.
Kwa Alliance waliopata ni Joseph James, Godfrey Luseke na Samir. Waliomshindwa Kindoki ni Martin Kigi, Dickson Ambundo na nahodha Siraji Juma. Matokeo ya jana yanamaanisha kwamba Yanga itakutana na Lipuli mjini Iringa kwenye mechi ya nusu fainali ya michuano hiyo, mchezo ambao utabiriwa kuwa na ugumu wa aina yake.
Mshindi huyo atakutana na mshindi wa mchezo wa KMC na Azam katika hatua ya fainali ambayo bingwa atapata nafasi ya kushiriki Kombe la Shirikisho msimu ujao.
Kocha wa Yanga, Mwinyi Zahera alisema hawakucheza vizuri kwani walipata nafasi tatu wakatumia moja tofauti na wapinzani wao. Huku akikiri kwamba kiungo cha Yanga kilizidiwa kwani Alliance walikuwa wakicheza kwa presha na kusababisha mechi hiyo kwenda kwenye penalti zilizoamuliwa na Kindoki ambaye awali mashabiki wa Simba walikuwa wakikejeli kwamba ni shemeji wa Zahera ndio maana anambeba.
Kocha huyo amesisitiza kwamba watapambana kwa kila namna kushinda kila mechi kwenye FA kwani ndiko kwenye nafasi kubwa ya kupata tiketi ya michuano ya kimataifa. Hiyo ni kutokana na ugumu na ushindani uliopo kwenye ligi licha ya kwamba wanaongoza msimamo mbele ya Simba na Azam.
0 Comments