Kabla hata ya mtanange wenyewe kuanza, ilibainika wazi kuwa Derby della Madonnina iliweka rekodi mpya katika ligi ya Italia – Serie A kwa kuingiza mapato ya euro milioni 5.7 katika mauzo ya tiketi na kitalii.
Zaidi ya tiketi 4,000 zilinunuliwa na mashabiki wa nje ya Italia na wamesafiri kwa ajili tu ya derby hiyo maarufu kama #DerbyMilano. Na baada ya mechi kukamilka uwanjani San Siro, ni dhahiri kuwa mashabiki waliofika uwanjani waliondoka wakiwa na tabasamu.
Mtanange huo kati ya watani wa jiji AC Milan na Inter Milan ulikuwa na kila aina ya uhondo. Mwishowe, Inter iliibuka na ushindi na kuwapiku AC Milan katika nafasi ya tatu ya Serie A kwa ushindi wa kusisimua wa 3-2.
Inter wamefikisha mechi sita za derby ya Milan bila kupoteza hata moja na sasa wamewaruka watani wao hao hadi nafasi ya tatu na pointi 53, mbili juu ya Milan katika nafasi ya nne.
Nambari mbili kwenye ligi Napoli waliponea mapambano ya Udinese na kushinda 4-2 lakini kulikuwa na hofu ya kipa David Ospina kupata jeraha la kichwa.
Imeripotiwa kuwa uchunguzi wa kichwa umeonyesha yuko sawa lakini ataangaliwa kwa siku mbili zaidi.
Napoli wamepunguza pengo kati yao na vinara Juventus hadi pointi 15.
Juventus – bila ya shujaa wake wa Champions League Cristiano Ronaldo – walipata kipigo cha kwanza cha msimu katika Serie A walipozabwa 2 – 0 dhidi ya Genoa.
0 Comments