Windows

Penalti ya Milner yairejesha Liverpool kileleni

Liverpool wamerejea kileleni mwa Ligi ya Premier lakini walihitaji penalti ya dakika za mwisho yake James Milner ili kuepuka kuangusha pointi dhidi ya Fulham.

Huku wakiwa kifua mbele kupitia bao la Sadio Mane lake la 11 katika mashindano yote msimu huu, wageni hao walishindwa kuwaangamiza Fulham na wakawaruhusu kurejea mchezoni.

Mparaganyiko kati ya beki Virgil van Dijk na kipa wake Alisson ulimzawadia Ryan Babel bao la kusawazisha dhidi ya klabu hiyo yake ya zamani.

Kisha kipa wa Fulham akafanya madhambi kwa kumuwangusha Msenegal Mane kwenye eneo la hatari kwa hiyo Milner akahakikisha kuwa wanapata ushindi wa 2-1.

Liverpool sasa wanaongoza ligi na mwanya wa pointi mbili mbele ya Manchester City ambao wana mechi moja ya ziada.

Kwingineko, Chelsea ilipata pigo katika kinyang’anyiro cha nafasi nne za kwanza baada ya kuduwazwa na Everton 2 – 0 licha ya kutawala mchezo katika kipindi cha kwanza.

Kocha Maurizio Sarri amesema “Tulicheza vizuri sana katika kipindi cha kwanza kuliko mchezo mwingine wowote msimu huu kisha ghafla mwanzoni mwa kipindi cha pili tukaacha kucheza. Sijui ni kwa nini. Tulikuwa hatarini,” alisema Sarri.

Amesema tatizo lilikuwa la kiakili zaidi uwanjani na sio mfumo wala mbinu za mchezo.

Matokeo hayo yana maana kuwa timu hiyo ya Maurizio Sarri imekosa nafasi ya kutoshana pointi na nambari nne Arsenal na hivyo watabakia nafasi ya sita nyuma ya Manchester United.


Post a Comment

0 Comments