Windows

Walitazamiwa wahame kabla ya dirisha halijafungwa



Ishu ya kubaki au kuondoka ilihitaji kusubiriwa hadi kwenye dakika za mwisho za usajili wa Januari jana usiku na kwamba Janssen alikuwa miongoni mwa mastaa waliokuwa wakitajwa na kuhusishwa na kuhama timu zao katika siku hiyo ya kufungwa kwa dirisha la usajili.ADVERTISEMENT


DIRISHA la usajili la wachezaji kwa mwezi Januari lilitarajiwa kufungwa jana Alhamisi saa tano usiku.


Kwa siku ya jana yote tangu asubuhi kulikuwa na dili kibao ambazo zilitazamiwa kukamilika kabla ya muda huo haijakwisha na dirisha kufungwa.


Kutokana na kwamba England ndio ilikuwa siku yao ya mwisho kwa mambo hayo ya usajili, kuna dili kibao za wachezaji ambao zilitarajiwa kukamilishwa hiyo jana. Baada ya kushuhudia mastaa kama Alvaro Morata, Mousa Dembele, Manolo Gabbiadini na Cesc Fabregas kukamilisha uhamisho wao mapema tu bila ya kwenda na presha ya kuwahi dirisha lisifungwe, kuna wachezaji hao walitazamiwa kuhama timu zao wanazocheza huko England katika siku ya mwisho ya kufungwa kwa dirisha hilo. Je, wamehama au wamebaki?


Hii hapa ndio orodha ya wachezaji waliotazamiwa kuhama kwa siku ya jana kabla ya dirisha hilo la uhamisho wa Januari halijafungwa.






Marouane Fellaini (Man United kwenda China)


Manchester United waliripotiwa kuwa kwenye mazungumzo na timu moja ya huko China juu ya kumpiga bei kiungo wao Marouane Fellaini kabla ya dirisha la usajili halijafungwa hiyo jana. Mbelgiji huyo amekuwa kwenye kikosi cha Man United tangu 2013 na kwamba alikuwa mchezaji muhimu chini ya Jose Mourinho kabla ya kuanza kusugua benchi baada ya ujio wa kocha Ole Gunnar Solskjaer kwenye kikosi hicho. Man United jana waliripotiwa walikuwa wakikamilisha mazungumzo hayo kuwahi muda kabla ya dirisha kufungwa licha ya kwamba huko China wataendelea kusajili hadi Februari 28.




Vincent Janssen (Tottenham kwenda Real Betis)


Janssen hakuwa na mwisho mwema chini ya Kocha Mauricio Pochettino huko Tottenham Hotspur licha ya kwamba amekuwa akisumbuliwa na majeruhi mengi. Kutokana na hilo, kuna timu moja ya La Liga, Real Betis ilikuwa ikihitaji huduma ya fowadi huyo wa Kidachi na walikuwa tayari kuweka mezani mzigo wa Pauni 15 milioni kunasa huduma yake. Ishu ya kubaki au kuondoka ilihitaji kusubiriwa hadi kwenye dakika za mwisho za usajili wa Januari jana usiku na kwamba Janssen alikuwa miongoni mwa mastaa waliokuwa wakitajwa na kuhusishwa na kuhama timu zao katika siku hiyo ya kufungwa kwa dirisha la usajili.






Callum Hudson-Odoi (Chelsea kwenda Bayern Munich)


Mabingwa wa Ujerumani, Bayern Munich kwa muda mrefu kwa mwezi uliopita walikuwa wakiifukuzia huduma ya kinda wa Chelsea, Callum Hudson-Odoi. Kitu kilichokuwa kikiwapa nguvu Bayern ni utayari wa mchezaji huyo kwenda kujiunga na wakali hao wa Bundesliga. Winga huyo ambaye alifunga bao kwenye mechi ya Kombe la FA dhidi ya Sheffield Wednesday Jumapili iliyopita aliripotiwa kwamba angekamilisha uhamisho wake wa kwenda kujiunga na Bayern Munich kwenye siku ya mwisho ya kufungwa kwa dirisha la uhamisho wa Januari jana usiku.




Javier Hernandez (West Ham kwenda Valencia)


Wakati West Ham United wakihaha kutengeneza makali kwenye kikosi chao cha ushambuliaji, kumekuwa na ripoti kwamba straika wao Javier Hernandez angeachana na timu hiyo kabla ya dirisha la uhamisho wa Januari kufungwa. Kocha wa Valencia, Marcelino mapema wiki iliyopita alisema mshambuliaji huyo maarufu kama Chicharito anahitajika sana kwenye kikosi chake na hilo lilikuwa likiwekwa sawa kwamba huenda uhamisho wake ungefanikiwa kabla ya dirisha la uhamisho huo wa Januari kufungwa. Marcelino alisema kwamba mchezaji mwenyewe anataka kwenda Valencia. Je, uhamisho ulitokea hiyo jana?








Nicolas Otamendi (Man City kwenda Barcelona)


Vinara wa La Liga, Barcelona wamekuwa wakisaka beki wa kati katika dirisha la uhamisho wa Januari lililofungwa rasmi usiku wa jana na kwenye mipango yao kulikuwa na jina la Nicolas Otamendi wa Manchester City. Beki huyo Muargentina, Otamendi mambo yake yamekuwa magumu msimu huu huko Man City kutokana na kocha Pep Guardiola kumweka benchi, akiwa amemwaanzisha kwenye mechi saba tu za ligi. Kutokana na hilo, Otamendi alikuwa kwenye harakati za kukamilisha uhamisho wake wa kwenda Barcelona hiyo jana kabla ya dirisha halijafungwa na huo ni moja ya uhamisho uliokuwa ukisubiriwa kuona utatokea.






Olivier Giroud (Chelsea kwenda Ufaransa)


Straika, Olivier Giroud alikuwa na dili mbili mezani kwake katika kuelekea siku ya mwisho ya kufungwa kwa dirisha la usajili hiyo jana Alhamisi. Kwanza alikuwa na mpango wa kurudi kwao Ufaransa, lakini kulikuwa na ishu nyingine ya kubaki London, lakini akienda kujiunga na West Ham United. Kuwasili kwa Gonzalo Higuain huko Stamford Bridge kumbe mvuruga straika huyo wa zamani wa Arsenal na sasa kitu ambacho alikuwa akikiwaza ni kuachana tu na Chelsea, huku kila kitu kilipangwa kufahamika jana kabla ya dirisha halijafungwa kama atabaki au ataondoka zake akiachana na maisha ya huko Stamford Bridge.






Lazar Markovic (Liverpool kwenda Besiktas)


Lazar Markovic hayupo kwenye mipango ya Kocha Jurgen Klopp huko Liverpool na hilo ndilo lililomfanya apambane kuachana na timu hiyo hasa kwa siku ya jana iliyokuwa ya mwisho ya kufungwa kwa usajili huko England. Ripoti kutoka Uturuki zilidai kwamba Besiktas walikuwa kwenye mazungumzo ya kumchukua jumla winga huyo na hilo lilitarajiwa kukamilishwa jana kabla ya dirisha la usajili kufungwa. Staa huyo wa Mserbia mkataba wake huko Anfield utafika tamati mwishoni mwa msimu huu na hivyo alikuwa akipambana kwa nguvu zote kuachana na maisha ya Anfield kabla ya dirisha kufungwa.






Adrien Silva (Leicester City kwenda Monaco)


Hadi kufikia asubuhi jana Alhamisi, Leicester City walikuwa bize kwelikweli kukamilisha dili la usajili wa mkopo wa staa wa AS Monaco, Youri Tielemans. Dili hilo ambalo Leicester City walitazamiwa kulikamilisha kwenye siku ya mwisho ya kufungwa kwa dirisha hilo la usajili, lilitarajiwa kumhusisha pia Adrien Silva, ambaye angetimkia upande mwinine. Silva alitaka kuondoka hapo kwenye kujiunga na Monaco na Leicester City walipanga kutumia hiyo fursa kumchukua Tielemans na mazungumzo yalikuwa yakiendelea katika kuelekea saa za mwisho za kufungwa kwa dirisha la usajili.






Idrissa Gueye (Everton kwenda PSG)


Kiungo, Idrissa Gueye tayari alikuwa ameshajipanga kuachana na maisha ya Everton na kwenda zake kujiunga na mabingwa wa Ufaransa, PSG. Ripoti zinadai kwamba Everton alikataa ofa ya Pauni 22 milioni kutoka kwa mabingwa hao wa Ufaransa, lakini katika kuelekea usiku wa jana wa kufunga dirisha la usajili, hivyo chochote kingeweza kutokea. PSG wanahitaji kiungo wa kati na jana walitazamiwa kupeleka ofa nyingine nono kabisa kunasa huduma ya Msenegali huyo, akakipige kwenye kikosi chao.






Aboubakar Kamara (Fulham kwenda Uturuki)


Mambo yenye utata mwingi ya nje ya uwanja yanayomhusu mchezaji Kamara, yamewafanya Fulham kuwa na mpango wa kuachana naye katika siku ya mwisho ya kufungwa kwa dirisha la usajili. Klabu moja ya huko Uturuki, Yeni Malatyaspor imeripotiwa kuhitaji huduma ya mshambuliaji huyo mwenye umri wa miaka 23. Hata hivyo, usajili huo ulikuwa na hatihati kwa sababu kocha wa Fulham, Claudio Ranieri bado anamhitaji na itakuwa vyema kwake kama hatakuwa ameuzwa na mabosi wake hadi kufikia jana usiku.


Post a Comment

0 Comments