Mwanza. Michuano ya Kombe la SportPesa ilimalizika Jumapili ya wiki iliyopita huku ikishuhudiwa timu ya Kariobangi Shark ya nchini Kenya ikitwaa Ubingwa, lakini ukiachana na hilo moja ya klabu iliyoacha gumzo ni Mbao FC.
Klabu hiyo ilikuwa mara yake ya kwanza kushiriki michuano hiyo, huku ikiwa ni timu mwalikwa ambapo pamoja na kukosa ubingwa lakini kazi yake ilionekana pale Uwanja wa Taifa.
Ukiachana na rekodi ya kutopoteza mchezao ndani ya dakika 90, gumzo ilikuwa namna ilivyoweza kuitoa Gor Mahia iliyokuwa mabingwa watetezi kwa misimu miwili mfululizo. Chama hilo lilionyesha umwamba na kuziacha Simba na Yanga kwa mbali, pengine wadau na mashabiki wa soka nchini wanaweza wasiijue zaidi Mbao,ambapo Mwanaspoti inakuletea uhalisia wa maisha yake ili hata Gor Mahia ambayo inashiriki michuano ya kimataifa ijue ilifungwa na klabu gani.
ILIVYOANZA
Ilianza kimasihara pale mitaa ya Sabasaba wilayani Ilemala jijini Mwanza, ambapo wauza samani na Mbao walipokuwa wanamaliza shughuli zao jioni wanajikusanya na kucheza kuweka mwili wao fiti. Baadaye wakajawa na wazo la kuanzisha timu na jambo ambalo lilipita na mwaka 2005 wakaisajili timu iitwayo Mbao FC na kuanza kushiriki Ligi ya Wilaya kisha ikatwaa ubingwa wa mkoa wa Mwanza na safari yao ikaanza hapo.
Mwaka 2014 ilishiriki michuano ya Ligi ya Mabingwa wa Mikoa (RCL), ambapo huko haikufanya masihara na kuthibitisha ubora wake na kweza kupanda Ligi Daraja la pili (SDL). Mwaka huo neema iliendelea kuiangukia timu hiyo kwa kufanikisha kupanda Ligi Daraja la Kwanza (FDL) msimu wa 2015/16 na kuweza kushiriki vyema na kumaliza michuano hiyo katika nafasi ya nne kwa pointi 12.
Lakini licha ya kuwa nafasi ya nne Shirikisho la soka nchini (TFF) liliitangaza timu hiyo kupanda Ligi Kuu baada ya baadhi ya timu kwenye kundi C kupanga matokeo katika mechi zao za mwisho na kushushwa daraja. Timu ambazo zilishushwa Daraja kipindi hicho ni Geita Gold Sports iliyoinyuka mabao 8-0 JKT Kanembwa na Polisi Tabora iliyoilalua mabao 7-0 JKT Oljoro na kujikuta katika wakati mgumu.
Pamoja na bahati hiyo, wadau wengi hawakuamini kama Mbao ingeweza kufanya lolote kwenye Ligi Kuu kwani kipindi hicho haikuwa na nguvu yoyote tofauti na sapoti ya mashabiki wake. Hadi sasa ni msimu wake wa tatu katika michuano hiyo mikubwa nchini, lakini ushindani wake ni mkali haswa inapokutana na timu kubwa ikiwamo Simba na Yanga na mara nyingi hupata matokeo mazuri.
FAINALI ZA FA
Ushindani wake haukuanza juzi wakati wa michuano ya SportPesa, timu hii ikiwa ni msimu wake wa kwanza kushiriki Ligi Kuu, ilifanikiwa kufika fainali ya michuano ya kombe la Shirikisho (FA). Kipindi hicho ikiwa chini ya Kocha, Ettiene Ndayiragije (kwa sasa yupo KMC) iliweza kufanya vizuri na kwenye fainali hiyo wakikipiga dhidi ya Simba ilitolewa kwa mabao 2-1 mchezo uliopigwa Dodoma.
Kuanzia msimu huo wa 2016/17 Mbao ilijizolea umaarufu katika medani za soka nchini ambapo hadi sasa timu za Simba na Yanga zinaiheshimu sana pindi wanapokutana. Hata hivyo hadi msimu huu kwenye Ligi Kuu, Simba ikicheza na timu hiyo katika Dimba la Kirumba ,ilikubali kichapo cha bao 1-0 na kuendeleza ubabe wake kwa timu hiyo kongwe.
MAISHA YA KAWAIDA
Pengine Gor Mahia na timu zingine za Kenya ambazo zilikuwa zikishiriki michuano ya SportPesa zinaweza kufikiri Mbao ni timu kubwa sana kutokana na ushindani iliyouonyesha, kumbe hamna kitu.
Maisha ya Mbao ni ya kawaida sana, kwani muda mwingine hata mishahara huchelewa lakini wachezaji wenyewe tu hujituma na kutaka kujitangaza katika medani za soka ulimwenguni.
Mbao haina kambi rasmi, mara nyingine huwa Chuo cha Ualimu Butimba eneo ambalo ni tulivu na hakuna kelele haswa inapofika mechi za Simba na Yanga ambapo uongozi huwapeleka huko ili kuondoa muingiliano baina yao na mashabiki. Pia mara nyingine huweka kambi katika Chuo cha D.I.T kule Ilemela ambapo na huko utulivu ni wa uhakika na sasa wamevumbua kwingine maeneo ya Lumara walipopangisha nyumba.
Kwa kifupi maisha ya klabu hiyo ambayo kwa sasa ndio yenye mashabiki wengi ni ya kuunga unga tofauti na umaarufu wake uliokuwa nao kwa sasa.
POSHO NA MOTISHA
Unaambiwa Mbao mambo ya posho hakuna,wachezaji wanaishi kwa kukarimiwa tu na kupewa ukweli juu ya maisha yao ya soka kuhakikisha wanajituma ili kusaka soko. Hili linawekwa wazi na Mwenyekiti wake, Solly Njashi ambaye anasema hakuna chochote wanachowapa wachezaji tofauti na mishahara kikubwa ni kuwaweka wazi kuthamini kazi yao.
“Hatuna pesa, hakuna posho za motisha, tunachofanya ni kuwaambia ukweli, mfano haya mashindano ya SportPesa tuliwaweka wazi kuonyesha ushindani kwa sababu yanarushwa na televisheni nyingi duniani,” anasema Njashi.
SAPOTI YA MASHABIKI
Wakati Mbao inawasili Mwanza kutoka Dar esa Salaam kwenye mashindano ya Sportpesa, Jiji lilizizima kwa muda huku wafanyabiashara wakisimamisha shughuli zao kwa muda kutokana na mapokezi yalivyokuwa, huku shangwe zikiwa ni za kufa mtu.
Magari, pikipiki ndivyo vilitawala katika jiji la Mwanza kwenye mapokezi hayo na walipofika mitaa Sabasaba yalipo makazi yao wakaangusha bonge la pati na kuwachangia pesa kama pongezi. Mwenyekiti wa mashabiki hao, Mustapha Rajabu anasema kutokana na mwenendo mzuri wa timu yao inawapa hamasa zaidi kuendelea kuiunga mkono.
“Tutaendelea kuisapoti timu yetu popote,tuliianzisha wenyewe lazima tufe nayo,tuna imani kubwa na wachezaji pamoja na benchi la ufundi litatufikisha tunapotakam,”alisema Rajabu.
KUHUSU SPORTPESA
Kocha Mkuu wa klabu hiyo ,Ally Bushiri ‘Benitez’ anaweka wazi kuwa licha ya kushika nafasi ya nne, lakini malengo yao hayakutimia kwani walihitaji ubingwa.
Anasema sababu zilizowakosesha kombe ni uzoefu kwa vijana wake pamoja na kukosa bahati kwani mechi walizofungwa ilikuwa ni mikwaju ya penalti.
“Hatukufikia malengo licha ya kushika nafasi ya nne,tulitaka Kombe ndio sababu tulimtoa bingwa mtetezi ili kubeba taji hilo,”anasema Benitez.
WACHEZAJI WALA KIAPO
Nahodha wa timu hiyo, David Mwassa anasema baada ya kukosa kombe hilo msimu huu wanaomba wapate nafasi nyingine ya kushiriki michuano hiyo ili wabebe taji hilo. Anasema mafanikio yao kwenye michuano hiyo ni kutokana na kila mmoja kujituma na kujitambua kwani soka ndio kazi yao, hivyo mashabiki waendelee kutoa sapoti kwa matokeo yoyote.
KIPA BORA AJISHANGAA
Metacha Mnata ambaye alikuwa kigingi golini na hatimaye kuchaguliwa kipa bora wa mashindano, anasema hakutarajia kuchaguliwa katika nafasi hiyo kutokana na timu nyingi kuwa na nyota wengi wenye uzoefu.
0 Comments