Windows

Majanga: Sarri akalia kuti kavu Chelsea





Mara baada ya kutoka vyumbani Sarri aliwaambia waandishi wa habari kwamba labda ni yeye mwenyewe anayepaswa kulaumiwa kutokana na matokeo hayo baada ya awali kuwalaumu wachezaji wake kufuatia kipigo dhidi ya Arsenal.ADVERTISEMENT



KWA Maurizio Sarri, presha inapanda presha inashuka. Taratibu ameanza kukalia kuti kavu. Anaijua vema tabia ya Roman Abramovich ya kuondoka na kichwa cha mtu Chelsea ikitibua uwanjani, lakini Sarri hataki kufa peke yake. Anataka kuondoka na wachezaji wake klabuni hapo.


Juzi Jumatano Chelsea ilichezea kichapo cha mabao 4-0 kutoka kwa Bournemouth ugenini uwanja wa Vitality na imegundulika kwamba Sarri aliwafungia wachezaji wa Chelsea kwa saa zima katika vyumba vya kubadilishia nguo huku akiwafukuza wasaidizi wake akiwemo, Gianfranco Zola katika kikao cha dharura alichoitisha uwanjani hapo.


Sarri anayejulikana kwa tabia yake ya kuvuta sigara mara kwa mara alilazimika kuitisha kikao cha kibabe baada ya Chelsea kupokea kipigo hiki kikubwa zaidi katika Ligi Kuu tangu walipochapwa mabao 5-1 na Liverpool Septemba 1996.


Wachezaji wa Chelsea walizomewa na mashabiki wao waliosafiri kutoka London kushuhudia pambano hilo huku Sarri pia akishuhudia timu yake ikipoteza pambano la pili mfululizo ugenini baada ya kuchapwa na Arsenal 2-0 katika pambano jingine la mwisho ugenini.


Kwa matokeo hayo, Arsenal imesogea mpaka nafasi ya nne huku ikiwa na tofauti nzuri ya mabao ya kufunga na kufungwa na ingawa timu zote zina pointi 47 lakini pia Manchester United iliyorudi upya chini ya kocha wa muda, Ole Gunnar Solskajer imebakiza pointi mbili tu kuifikia Chelsea ambayo awali ilikuwa na pengo kubwa la pointi dhidi ya United.


Mara baada ya kutoka vyumbani Sarri aliwaambia waandishi wa habari kwamba labda ni yeye mwenyewe anayepaswa kulaumiwa kutokana na matokeo hayo baada ya awali kuwalaumu wachezaji wake kufuatia kipigo dhidi ya Arsenal.


“Labda ni kosa langu, labda nashindwa kuwahamasisha lakini timu ni imara na pia inaweza kushinda bila ya kocha. Inabidi tuseme samahani kwa mashabiki wetu. Tunaweza kupoteza mechi, sawa, katika kila mechi, lakini sio kwa staili hii. Inabidi tutatue hili tatizo. Inabidi tuelewe tatizo lipo wapi.” Alisema Sarri.


Mashabiki wa Chelsea uwanjani walionyesha hasira zao kwa kocha huyo aliyechukuliwa kutoka Napoli ya Italia katika kipindi cha majira ya joto kuziba nafasi ya Antonio Conte huku wakiimba kwa kusema ‘Haujui unachofanya’.


Katika pambano hilo Sarri alimuanzisha mshambuliaji wake mpya wa kimataifa wa Argentina, Gonzalo Higuain ambaye hata hivyo alishindwa kuonyesha makali katika pambano hilo la kwanza kwake Ligi Kuu ya England na nafasi yake ilichukuliwa na Olivier Giroud katika kipindi cha pili.


Hiyo ni mechi ya pili kwa staa huyo aliyechuliwa kwa mkopo kutoka Juventus kucheza huku pambano lake la kwanza likiwa dhidi ya Sheffield Wednesday wikiendi iliyopita katika michuano ya FA na mpaka sasa anahaha kusaka bao lake la kwanza Chelsea.


Sari alimpiga benchi kinda mahiri wa timu hiyo, Callum Hudson-Odoi kwa kile kilichosemekana kumuadhibu baada ya kinda huyo kuandika barua ya kutaka auzwe katika dirisha la Januari huku Bayern Munich wakiwa tayari kutoa dau la Pauni 40 milioni kwake.


Chelsea pia inaanza kupitia katika nyakati ngumu baada ya Sarri kukiri kabla ya pambano hilo kwamba staa wao wa kimataifa wa Ubelgiji, Eden Hazard anataka kuondoka klabuni hapo huku Real Madrid wakionyesha nia ya kumchukua katika dirisha kubwa lijalo la majira ya joto.


Hazard amegoma kusaini mkataba mpya Stamford Bridge na kuna uwezekano mkubwa Chelsea imemnasa winga wa Borussia Dortmund, Christian Pulisic kwa ajili ya kuwa mbadala wake.




ADVE

Post a Comment

0 Comments