Windows

WACHAWI WA DAR WAMEONDOKA NA MAHADHI, HAWAJAMRUDISHA WAMEMBEBA NA SALAMBA...!!!



Na Saleh Ally
NINGESEMA ninaandika barua ingekuwa ni jambo zuri sana lakini acha iwe katika mfumo wa makala na sasa nawagusa wachezaji wawili tu wa Yanga na Simba ambao wanaweza kuwa wawakilishi wa wengine.


Ninataka kumzungumzia Adam Salamba lakini siwezi kufanya hivyo bila ya kumgusa Juma Mahadhi, wachezaji makinda na Watanzania wenzangu ambao ninaamini wana bahati ya kupata kipawa kutoka kwa mwenyezi Mungu.



Najua hakuna anayeweza kukataa kwamba Mahadhi na Salamba ni vijana wenye vipaji vya mchezo wa soka. Wanaweza kuwa wana vipaji vingine lakini sivijui na ningependa kulalia katika soka zaidi ambacho ndio muhimu zaidi.

Wakati Mahadhi anasajiliwa na Yanga akitokea Coastal Union, hakuna ubishi matarajio ya wadau wengi yalikuwa makubwa na tuliamini atafanya vema hata kama ni baada ya muda fulani.


Tuliona juhudi za kocha George Lwandamina ambazo hakika zilikuwa ni za kupewa kongole. Alijitahidi kadiri ya uwezo wake kumpa nafasi kwa lengo la kuona anakuwa msaada, hata hivyo msaada ulikuwa mdogo sana.

Baada ya muda, Mahadhi ameingia katika majeruhi ya muda mrefu na mwisho hiki ndiyo kimegeuka kisingizio. Lakini binafsi ninakumbuka kabla ya kuumia, bado nafasi yake ilikuwa finyu na alipopewa nafasi hakufanya vema.

Sasa Mahadhi ni kati ya wachezaji wa kawaida Yanga, wachezaji wasio na muhimu sana na wachezaji ambao kama Yanga ikitaka kupunguza gharama basi hawawezi kuwa na nafasi ya kung'ara.


Huko Simba yupo Salamba ambaye hana tofauti kubwa kiumri na Mahadhi, hana tofauti kubwa na namna walivyosajiliwa, kwamba baada ya kutamba Lipuli FC, Simba wakafanya juhudi ya kumpata na wakaeleza kwamba wanamhitaji awe msaada msaidizi huku akizoea kwa kuwa tayari wana magwiji pale mbele.


Alivyoanza ilikuwa vizuri sana, bila shaka ni kama Mahadhi, amekwenda vizuri lakini sasa ukisikia hata benchi hana nafasi si jambo la ajabu kwa kuwa hana nafasi ya kucheza na kinachoshangaza, Simba ina wachezaji walewale. Sasa vipi Salamba atoke kupata namba ya kucheza akose hata nafasi ya kukaa benchi tena kwa kipindi kifupi tu cha ndani ya miezi mitatu?


Tukubali hisia za kipuuzi za "wamepigwa misumari", tukubali kuwa wajinga kuonyesha tunaamini ushirikina na hisia za kipuuzi kwamba hawafanyi vizuri kwa kuwa wameendewa kwa waganga?

Vipi hawawaendei kwa waganga akina Emmanuel Okwi, Meddy Kagere au Heritier Makambo na wenzao? Lakini kweli dalili zinaonyesha wameendewa kwa wanganga?



Ninahoji hili kwa kuwa nilizungumza na mdau mmoja ambaye alitumia dakika zake nne kunieleza mambo mengi ya kipuuzi akitaka kunivuta kuamini eti wachezaji kadhaa wamefanyiwa ushirikina ndio maana wanaumia kila mara.


Huyu mtu hakuwahi kunionyesha uhakika kama kweli Salamba au Mahadhi na wachezaji wengine wa aina hiyo wamekuwa wakipumzika vya kutosha, hawashiriki starehe kwenda klabu, kuchelewa kulala, kunywa pombe au kujikita na furaha za wanawake.



Inakuwaje hawa hawakurogwa Iringa na Tanga, waje warogwe Dar es Salaam? Uchawi wa Dar es Salaam ni starehe, ulimbukeni, kulewa sifa au kuwa na pupa za kipuuzi ambazo zimewaangusha wengi baada ya kuliingia jiji vibaya.

Si unajua, Dar es Salaam kuna warembo kuliko mji wowote katika nchi hii? Baa nyingi na zinazovutia kuliko sehemu yoyote. Unajua, Dar es Salaam haiwezi kuwa kama Tanga au Iringa.

Kufanya kazi Dar es Salaam lazima uwe na nidhamu maradufu kwa kuwa vishawishi vilivyopo vina uwezo wa kushawishi hata kuliko shetani mwenyewe na usisahau kuna watu kama wapambe ambao wanaishi kwa upambe.
Kawaida wapambe wanasubiri wengine watafute halafu wao wawashirikishe katika matumizi kwa kuwa watawaitia mademu, watawaonyesha sehemu nzuri za baa fulani, kumbi za disco na kadhalika.


Sisemi hawa wamepita huko lakini inawezekana wameguswa na mwendo huu wa njia zisizo sahihi na ikiwezekana wana uchovu bado unaowafanya washindwe kuamka na bahati mbaya waliowazunguka wanaweza kuwa si wakweli kwao.
Kwamba kama kuna tatizo fulani, mchezaji analalamika na unaona hayuko sahihi na wewe ni mtu wake wa karibu unajaribu kuwa mpambe badala ya mkweli. Tena inawezekana ukawa mpambe wa kumpeleka kwa waganga wa kienyeji akajimalize kabisa.


Soka la Ulaya ndio limeendelea zaidi kuliko sehemu nyingine duniani na hatusikii umahiri wa waganga. Badala yake ni misingi sahihi kama ya utendaji kazi na kuwa makini.


Hivyo Salamba, Mahadhi na wengine ambao wamekuwa wageni wa Dar es Salaam kwa maana ya kipindi cha kuwa wana kazi na fedha, lakini pia ni maarufu, wajichunge na kujiangalia upya kwa kuwa mategemeo ya kufanya vizuri unaposajiliwa lazima yawepo, ukifeli ujue unawafelisha na kuwaangusha wengi wakiwemo ambao walitarajia makubwa.



Inawezekana kubadili gia na mambo yakaenda lakini ili kubadili lazima mhusika akubali kuwa, mchawi wake namba moja ni yeye mwenyewe.

Post a Comment

0 Comments