HABARI kubwa kwenye Ligi ya Wanawake Tanzania maarufu kama Serengeti Lite Women's Premier League ni timu ya JKT Queens ambao ni mabingwa watetezi wa kombe hili.
Mpaka sasa wamecheza michezo tisa wanaongoza ligi wakiwa wamejikusanyia pointi 27 na hawajapoteza mchezo hata mmoja.
Spoti Xtra imefanya mahojiano na Kocha Mkuu wa JKT Queens, Ally Ally ili kujua hesabu zake na mipango ndani ya kikosi huyu hapa anafunguka:-
"Ligi msimu huu ni ngumu kila timu inapambana kutafuta matokeo, jambo hilo linatufanya tukomae kwenye mechi zetu tunazocheza kwa sasa.
"Timu ina pambana uwanjani na kila mchezaji anatimiza jukumu lake.
"Wachezaji wanajua kutumia makosa ya wapinzani, akili wakiwa uwanjani na mbinu ngumu ambazo ninawapa, wanajua ligi ni ngumu na wao wanapaswa kuwa wagumu.
Siri ya mafanikio inabebwa na nini?
"Nidhamu ya wachezaji kuelewa kile ninachowaambia na wanafanya kwa vitendo wakiwa uwanjani, hakuna jambo jingine zaidi ya wao wenyewe kuamua kubadili matokeo.
"Wote wanacheza wakiwa ni timu wanashirikiana kutafuta matokeo kwa ajili ya timu na matokeo hayajifichi.
"Wachezaji wangu wana uzoefu na Ligi ya wanawake hivyo inakuwa rahisi kwao kupata matokeo.
Mechi ipi kwako ilikuwa ngumu?
"Mchezo wangu na Simba haukuwa mwepesi, ni mchezo ambao ulinifanya nijue uwezo wa wachezaji wangu binafsi mbali na kile ninachowafundisha, walifanya kazi kubwa na wakapata matokeo.
Kwa nini Simba?
"Nimepata taabu kupata matokeo kwa Simba, ukiangalia timu nyingi nilizocheza nazo nilifanikiwa kushinda mabao zaidi ya matatu ila kwa Simba nilipata bao moja hii inamaanisha ni timu ngumu na bora.
"Pia wao walikuwa nyumbani unajua nyumbani ni nyumbani tu walileta ushindani wa kweli, pia timu ya Alliance Girls nayo ni miongoni mwa timu bora, imani yangu timu zote ni bora ndani ya ligi na ninaziheshimu.
Malengo ya timu kwa sasa yanaegemea wapi?
"Kulitwaa kombe huko ndiko hesabu zilipo, hakuna jingine kwa sasa ndani ya kichwa changu na timu yangu.
"Sisi ni watetezi tunatakiwa tufanye kweli tubebe kombe letu turejee nalo tena nyumbani.
Mmekusanya mipira mingapi kutokana na wachezaji wako kupiga 'hat-trick'?
"Wachezaji wangu wawili wana mipira yao ambayo imetokana na kufanya hivyo ni jambo la kujivunia kwao na kwa timu pia ila imani yangu wanapaswa wapewe mingi zaidi ya hii kwa sababu wanafanya kazi kubwa Uwanjani.
Kabla ya mchezo unawaambia nini wachezaji wako?
"Tunatafuta ushindi sisi ni mabingwa watetezi tucheze kwa nidhamu kupata matokeo uwezo upo mikononi mwetu.
"Dua kabla ya mechi na baada ya mechi ni muhimu kwetu.
Kuna utofauti gani wa Ligi ya msimu huu na msimu uliopita?
"Mwaka huu kuna ule mwamko kwa mashabiki angalau tofauti na msimu uliopita kutokana na msisimko ambao upo kwa mashabiki wenyewe.
"Bado tuna nafasi ya kufanya vizuri endapo nguvu kubwa itawekezwa na kila mmoja akapenda kutoa sapoti kwa timu.
Uwepo wa mdhamini Serengeti Lite unauzungumziaje?
"Wameonyesha njia kwa wengine na ni muda wa kuwekeza zaidi kwenye soka la wanawake kama ambavyo Serengeti Lite wameanza ni muda wa kufikia mafanikio ambayo tunayafikiria.
"Bado uhitaji ni mkubwa ukizingatia kuendesha ligi ni gharama.
Ugumu wa mashindano unakwamisha na nini?
"Ratiba ya ligi haipo sawa kwetu, yaani wachezaji hawapati muda wa kupumzika kwa mfano Jumatano una mchezo Mwanza jumapili tena unakuwa Dar, hapo unakuta wachezaji hawapati muda wa kupumzika ukizingatia ni watoto wa kike.
Timu yako inafunga mabao mengi muda mwingine mpaka 10 kwa nini?
"Ubora wa timu niliyonayo pamoja na mfumo ambao ninautumia.
"Nimecheza michezo tisa sijapoteza hata mchezo mmoja na kibindoni nina ponti 27 nafasi ya kwanza," anamalizia Ally.
0 Comments