Windows

WAWILI TEGEMEO SIMBA WAONDOLEWA KIKOSINI, YUPO MKUDE


Kiungo mkabaji wa Simba, Jonas Mkude na beki wa pembeni wa timu hiyo, Mohammed Hussein ‘Tshabalala’, wameondolewa kwenye orodha ya kikosi cha timu hiyo kitakachoivaa Al Ahly ya Misri.

Simba inatarajiwa kuwavaa Al Ahly katika mchezo wa hatua ya makundi ya Ligi ya Mabingwa Afrika utakaopigwa huko nchini Misri. Katika mchezo huo, Simba inatakiwa kupata ushindi au sare ya aina yoyote ili wajiwekee mazingira mazuri ya kusonga mbele katika hatua inayofuata ya michuano hiyo.

Katika mazoezi ya mwisho ya timu hiyo yaliyofanyika jana asubuhi kwenye Uwanja wa Boko Beach Veteran jijini Dar es Salaam kabla ya jioni kuanza safari ya kuelekea Misri, kocha wa Simba alijaribu kupanga kikosi tofauti na kile kilichozoeleka.

Kwenye mazoezi hayo, Kocha Mkuu wa timu hiyo, Mbelgiji, Patrick Aussems alipanga vikosi viwili vya timu hiyo na kucheza mechi ya mazoezi baada ya kumaliza mazoezi ya mbio fupi, ndefu na viungo.

Mbelgiji huyo alipanga vikosi viwili vya timu hiyo huku kimoja kikionekana ni kile atakachokitumia katika kikosi cha kwanza huku wawili wakiondolewa na kuingia wawili walioanzia benchi mchezo uliopita dhidi ya AS Vita ya Kinshasa, Congo.

Wachezaji waliongia katika kikosi cha kwanza ni winga chipukizi Rashidi Juma na beki wa pembeni Mghana, Asante Kwasi aliyerejea nchini Jumamosi iliyopita akitokea nyumbani kwao Ghana.

Wakati mazoezi hayo yakiendelea, Mbelgiji huyo alionekana muda mwingi akitoa maelekezo kwa wachezaji waliokuwa wanaunda kikosi cha kwanza ambao anaweza kuwaanzisha katika mchezo huo ambacho kilikuwa hivi;- Aishi Manula, Nicholas Gyan na Asante Kwasi. Wengine ni Pascal Wawa, James Kotei, Rashid Juma, Hassani Dilunga, Meddie Kagere, Clatous Chama na Emmanuel Okwi.

Mechi hiyo ya mazoezi ikiendelea, Mbelgiji huyo alionekana akitoa maelekezo kwenye kikosi hicho chake cha kwanza atakachokitumia huku wakati mwingine akionekana kusimamisha mazoezi na kutoa maelekezo.

Akizungumzia hilo, Mbelgiji huyo alisema: “Kikubwa naendelea kukifanyia marekebisho kikosi changu kwa kuangalia baadhi ya upungufu niliouona kwenye mchezo uliopita na AS Vita. 

“Hivyo, ni lazima kikosi changu kiwe na marekebisho na nimemuingiza Kwasi katika msafara wangu, ni baada ya kujiaminisha kuwa kwao Ghana alikuwa akifanya mazoezi gym, hivyo sina wasiwasi naye.”

CHANZO: CHAMPIONI

Post a Comment

0 Comments