BAADA ya mashindano ya SportPesa Cup kukamilika wikiendi iliyopita, Ligi Kuu Bara ambayo ilisimama kwa muda inatarajiwa kuendelea wikiendi hii.
Kwa kilichotokea SportPesa Cup ni aibu kiujumla kwa Taifa hivyo timu zote za Tanzania zitambue kwamba zimeshindwa kwa mara ya pili nyumbani kuonyesha ukomavu wao hivyo wachukue kama funzo.
Turudi kwenye Bodi ya Ligi Kuu Bara Tanzania (TBLB) inayofanya kazi sambamba na Shirikisho la Soka Tanzania (TFF) itazame kwa umakini namna ya kupanga ratiba ya Ligi Kuu Bara.
Katika ratiba hiyo inaonyesha kuna baadhi ya mechi za viporo kwa baadhi ya timu zitachezwa Aprili mwaka huu kitu ambacho naona ni mbali wakati hapa kati kuikuwa na uwezekano wa mechi hizo kuchezwa.
Uwepo wa viporo kwa timu unaua msisimko wa Ligi Kuu Bara ni lazima kuwe na uwiano wa michezo hata kama kuna viporo basi visizidi sana.
Katika jambo ambalo linavuruga ratiba ni pamoja na viporo maana kuna wakati timu zina nafasi ila hakuna mchezo unaochezwa kwa kile kinachoelezwa ni timu kucheza michezo ya kimataifa.
Wahusika inabidi hili mliangalie kwa jicho la kipekee namna itakayokuwa bora kwa timu zote kuwa na uwiano kuondoa dhana ya timu fulani kubebwa na nyingine kukandamizwa.
Wimbo huu umekuwa ukiimbwa mara nyingi huku viongozi wakionekana kuendelea kurudia yaleyale ambayo yanasemwa jambo ambalo linaendelea kuleta ukakasi kwenye Ligi yetu.
Kuna timu sasa zinaviporo mpaka mechi sita huku wengine wakibaki na kiporo kimojakimoja hii sio sawa kwa utaratibu ukiangalia kuna nyingine zimecheza zile zinazotakiwa.
Hivyo wahusika mkicheza vizuri na ratiba itafanya ligi iwe bora na yenye ushindani mkubwa kila iitwapo leo ndani ya Tanzania na kufanya tupate washindi makini.
Nichukue nafasi hii kuzikumbusha timu kwamba mzunguko huu wa pili timu zote zinatakiwa zijipange sawasawa maana ligi hii ni ya mwenye kisu kikali ndiye atakula pointi tatu ukizubaa unaachwa.
Benchi la ufundi pamoja na viongozi ni muda wa kutazama makosa ambayo mmeyafanya kwenye mzunguko wa kwanza. Mzunguko huu wa lala salama suala la makosa msilipe nafasi.
Mkishatambua mnapokoesa hapo ndipo pa kuanzia ili kuleta ushindani wa kweli ndani yaligi katika michezo yenu yote mtakayocheza iwe nyumbani ama ugenini.
Ushindani uwe mkubwa zaidi ya mwanzo kwani kwa sasa mzunguko huu ni mgumu kuliko ule wa awali ambao kila timu ilikuwa ina matumaini ya kupata ushindi.
Kumbukeni mnapoingia uwanjani ondoeni ondoeni akili ya kuwa hii ni timu ndogo na hii ni timu kubwa mkiwa na akili hiyo mtapata matokeo msiyoyatarajia.
Duniani kote hakuna timu ndogo wala kubwa mnapokuwa kwenye mashindano sawa basi nyie wote levo yenu ni moja,.Hakuna nafasi ya dharau katika soka.
Nimezungumzia hilo kutokana na kushuhudia timu kadhaa zikicheza kwa kiwango cha juu pale zinapokutana na timu kama Azam FC, Yanga, Simba lakini zinapocheza na nyingine hali inakuwa tofauti zinakuwa kawaida kwa maana ni saizi yao hilo sio sawa.
Mnapoamua kupambana basi hakikisheni mnafanya hivyo kwa timu zote ili kufikia malengo yenu. Kumbukeni mnapoingia uwanjani mkiwa na akili kwamba mnakutana na timu kubwa hamtaweza kufikia malengo yenu.
Unapocheza vizuri kwa juhudi unapata matokeo chanya yatakayokufanya uwe sehemu bora na kuepuka hali ya kushuka daraja msimu huu.
Kila timu ina nafasi ya kushinda endapo itaamua kutafuta ushindi ndani ya Uwanja kwa wachezaji kupambania timu
zao.
Kutoka Championi
0 Comments