KIKOSI cha Simba kiliwasili salama nchini Misri na leo watafanya mazoezi ya mwisho nchini humo kabla ya kuwavaa Waarabu wa Al Ahly katika mechi ya tatu kwenye kundi 'D' Ligi ya Mabingwa katika hatua ya makundi ambayo itachezwa saa 3:00 usiku kwa saa za Afrika Mashariki.
Katika kuhakikisha mambo yanakuwa mazuri kwa upande wa Simba kocha wa timu hiyo alisema kwanza matokeo ya kufungwa 5-0 dhidi ya AS Vita katika mechi iliyopita yamekuwa kama fundisho kubwa katika kikosi chake haswa katika mechi na Al Ahly.
Aussems alisema hali ya hewa iliyokuwa Misri ni ya baridi tofauti na ambayo ipo hapa Dar es Salaam, ndio maana wamewahi zaidi ya siku tatu ili kuzoea mazingira na hali ilivyo nchini humo na mpaka siku ya mechi watakuwa wamezoea.
Anasema hali ya hewa inaweza kuwa faida kwa wapinzani lakini kuwahi kuja hapa mapema, ni faida hata kwetu tofauti na tungefika hapa nchini siku moja kabla ya mechi.
"Hakuna timu ambayo inakwenda kushindana na ikakubali kuwa wanakwenda kupoteza hapana, na ili kuhakikisha tunapata matokeo yanye faida kwetu tulianza kufanyia kazi makosa ya kutokuba mpaka mwisho ambayo yalichangia kupoteza mechi iliyopita," alisema.
"Tulipata muda mzuri tukiwa kwetu Tanzania kufanya mazoezi ya kutosha lakini huku tulipo hali ya hewa ni tofauti kabisa na ambapo tumetoka lakini tutajitahidi kuzoea ili kwenda kushindana na kupata kile ambacho timu imekusudia.
"Najua tunacheza mechi mbili mfululizo ugenini lakini katika mchezo huu wa kesho tutacheza tofauti na vile ambavyo tulionekana katika mechi na AS Vita kutakuwa na mabadiliko ya kiuchezaji kulingana na tulivyowaona wapinzani, na hilo tumelishalifanyia kazi mazoezi.
"Natambua tunakwenda kucheza mechi na timu ngumu ambayo ni bora Afrika lakini katika kikosi changu ili kuweza kushindana nao kutakuwa na mabadiliko ya wachezaji tofauti na kilivyoanza katika mechi iliyopita na AS Vita," alisema Aussems.
MKUDE AMTIBUA MBELGIJI
Kikosi cha Simba kilifanya mazoezi ya mwisho hapa nchini siku ya Jumanne ambayo jioni yake walianza safari ya kwenda Misri lakini kiungo mkabaji wa timu hiyo Jonas Mkude alikuwa kama amemtibua kocha wa timu hiyo Aussems.
Ilikuwa hivi, mazoezi ya Simba yalianza saa 3:30 asubihi lakini mpaka mazoezi hayo yanaelekea ukingoni Mkude alikuwa hajaonekana na kumfanya kocha wa timu hiyo kukerwa na jambo hilo na alionekana kuwa mkali.
Muda mfupi kabla ya mazoezi kumalizika Mkude alifika mazoezi hapo na kufanya mazoezi akiwa peke yake huku akisimamiwa na kocha wa viungo Adel Zrane muda mfupi tu kabla ya mazoezi kumalizika.
"Aussems alikuwa amekasilika sana na kama Mkude asingekuja mazoezini asingekuwa sehemu ya kikosi ambacho kipo Misri na kama uliona vizuri katika nafasi yake katika mazoezi alicheza Hassan Dilunga," alisema kigogo mmoja wa Simba.
0 Comments