KATIKA hali isiyo ya kawaida tumeshuhudia tena kwa misimu mitatu mfululizo kombe la SportPesa Cup likibebwa na timu ya Kenya hii ni aibu kubwa kwa Taifa letu la Tanzania.
Ikumbukwe kwamba mwaka 2017 wakati mashindano yanaanza yalichezwa nchini Tanzania ambapo timu zetu Simba, Yanga, Singida United zilikuwa ni miongoni mwa zilizotuwakilisha ila zote ziliboronga.
Ziliruhusu kombe kubebwa katika ardhi ya Tanzania na kwenda kwa Gor Mahia, ikawa hivyo tena mwaka 2018, Simba, Yanga na Singida United zilishiriki nchini Kenya kombe likabaki kwa Gor Mahia.
Safari hii imefanyika tena Tanzania, Simba, Yanga, Singida United na Mbao zimeshiriki kombe limekwenda Kenya kwa KK Sharks baada ya kuwafunga Bandari bao 1-0 kwenye mchezo wa fainali.
Simba na Yanga ambazo ni timu kongwe zilitarajiwa kufanya kweli msimu huu zote hamna kitu pamoja na Singida United ambayo kila mara ilishiriki.
Niipongeze timu ya Mbao FC ambayo hii ni mara yake ya kwanza kushiriki na imeleta ushindani wa hali ya juu na kumaliza nafasi ya nne na kujinyakulia dola 5,000.
Sidhani kama kuna cha kujitetea kwenu kwa hichi mlichokifanya mwaka huu. Mashindano yamekuja katikati ya Ligi Kuu Bara mkiwa na vikosi vyenu kamili.
Kipindi kile mlikuwa mnadai wachezaji wapo likizo wakati michuano ilipokuwa inafanyika mwisho mwa msimu hali iliyofanya msifanye vizuri,Sasa mtajitetea na nini.
Mnatakiwa kutambua kwamba mmewaumiza mashabiki wenu wanaowapa sapoti mnapokuwa uwanjani.
Simba wamefanya jambo ambalo halina tofauti sana na Yanga hasa kwa mashabiki wao hivyo hivi sasa mna deni kubwa sana kwa mashabiki wenu na wote mnatakiwa kuwaomba radhi mashabiki kwa kushindwa kutwaa ubingwa.
Nasema Simba kwa sababu wao wana kikosi kipana chenye wachezaji wengi wazuri na wenye uwezo sasa hali ya kutafuta sababu inaleta maswali hasa kwa mashabiki na taifa kiujumla.
Hakuna shabiki anayependa kuona timu yake inafanya vibaya, inapofikia hatua timu inaboronga ni lazima viongozi wachukue hatua za haraka kuweka mambo sawa na kumfanya shabiki kutoa sapoti.
Mbali na hilo pia Simba mnatakiwa mtambue kwamba mnaiwakilisha nchi katika mashindano ya kimataifa sasa mtawezaje kuleta ushindani ilihali huku mambo yanaanza kwenda kombo?.
Bado kuna kazi kubwa kwa viongozi kuangalia namna mnavyofanya usajili mnapaswa kuwapa majukumu yote muhimu benchi la ufundi pamoja na taatibu za kufuatwa.
Hili suala la wachezaji wa Simba kudaiwa kutoroka kambini uongozi unaweza kufikiria ni jambo dogo ila lina athari kubwa kwa mashabiki pamoja na wachezaji pia hapo baadaye.
Tayari limeanza kuonekana ingawa viongozi wanaweza wakajifanya hawajaona namna ilivyokuwa kwenye mchezo wa kumtafuta mshindi wa tatu, hakuna shabiki wa Simba aliyekuwa na furaha ya kweli anaamini hapati kile ambacho anastahili kutoka kwa wachezaji wake.
Mashabiki wanaipenda timu yao ila wanavunjwa moyo na matokeo mabovu mfululizo bila kutwaa kombe lolote lile hawezi kuwa na furaha ya kweli katika hali kama hii.
Kuhusu mikakati ya kuwalinda wachezaji hakuna kitu kama hicho hasa kwa mchezaji mkubwa alindwe vipi kwani yeye mtoto suala la muhimu kujiuliza je wanajitambua wachezaji wenyewe?
Wanajua majukumu yao na wamepangiwa majukumu yao kikamilifu, mkataba wao unazungumza nini? Kila mmoja ana haki zake sasa kama mnataka mchungwe mkiwa kambini je mkiwa nje ya kambi itakuaje?
Umuhimu upo kwa wachezaji kujitambua na kufanya kazi kwa moyo mmoja kazi yao ni kucheza mpira hayo mambo mengine yanakuja. Kikubwa kilichopo kwa sasa kwa Simba ni kuona namna gani wanaweza kuboresha nidhamu kwa wachezaji.
Mataji matatu ambayo Simba wamepishana nayo mpaka sasa ni ya maumivu kwa mashabiki hivyo wachezaji wanapaswa kuwaomba msamaha na kufanya kazi kwa vitendo.
Mpaka sasa Simba wamepishana na vikombe vitatu ambavyo ni Kombe la FA, Kombe la Mapinduzi pamoja na kombe la SportPesa Cup sasa hapo unadhani mashabiki mtawaambia nini kama sio kubadilika na kufanya kazi kwa vitendo.
Wachezaji hivi ni nini ambacho mnakikosa ndani ya Simba? Mashabiki hawahitaji mambo mengi wao wanahitaji ushindi na vikombe hicho ndio kipaumbele chao na mkifanya hivyo mtakwenda nao sawa.
Hivi sasa mnakwenda nchini Misri kucheza mchezo wa Ligi ya Mabingwa Afrika na Al Ahly ukiwa ni mchezo wa tatu, sasa fanyeni kweli ilikurejesha imani kwa mashabiki fanyeni kweli.
Kitendo cha kufungwa mabao 5-0 kiliwashangaza wengi hivyo badilikeni fanyeni kweli lisije likajirudia.
Kutoka Championi
0 Comments