

USHINDI wa mabao 2-1 waliopata Simba dhidi ya AFC Leopard ya Kenya katika mashindano ya Kombe la SportPesa umewapeleka hatua ya nusu fainali ambapo sasa watacheza na Bandari FC ya Kenya.
Mechi hiyo iliyochezwa jana Jumatano jioni Uwanja wa Taifa jijini Dar es Salaam, Simba ndiyo ilikuwa ya kwanza kupata bao kupitia Emmanuel Okwi dakika ya 13 akiunganisha krosi ya Zana Coulibaly ndani ya boksi akiwapiga chenga mabeki wa Leopards.
Baada ya kupata bao hilo, Simba waliongeza kasi ya kushambulia ingawa walipoteza nafasi nyingi walizozipata huku, Haruna Niyonzima alimuwekea pasi safi ya mzungusho (Kibao) Okwi ambaye alikutana uso kwa uso na kipa wa Leopards, Adira Jairus ambaye aliupangua mpira huo.
Wachezaji wapya wawili wa Simba, beki Lamine Moro alionekana kutulia na kucheza kwa maelewano mazuri na Pascal Wawa wote wakiwa wanacheza nafasi ya ulinzi wa kati, Moro alikuwa akianzisha mipira kwa Coulibaly, beki wa kushoto Rashid Juma na viungo wa kati Jonas Mkude na Niyonzima.
Kwa upande wa straika mpya Emmanuel Kassimbo alikuwa bora katika kupokea mipira ambayo ilitoka kwa viungo, ingawa umiliki wake wa mpira haukuwa mzuri.
Kassimbo mpaka kipindi cha kwanza kinamlizika hakupiga shuti lolote la hatari zaidi ya kuruka kichwa ambacho kilitokana na krosi ya Okwi na hakikuwa na hatari yoyote.
Kassimbo hakuwa mwenye hatari zaidi kipindi chote cha kwanza pengine kama ilivyotarajiwa na wapenzi wa Simba kutamani kumuona hata akiwa anafunga bao.
Simba walianza kufanya mabadiliko kipindi cha pili walitoka Wawa, Mkude, Kassimbo, Okwi na Hassan Dilunga waliingia Maddie Kagere, Juuko Murushid, James Kotei, Mzamiru Yasin na Mohamed Ibrahim.
Leopards wao hawakuwa na mashmbulizi ya mara kwa mara ndani ya dakika 45 za kipindi cha kwanza na walikuwa wakishambulia kwa kushtukiza.
Dakika ya 48 kipindi cha pili Simba walifanya shambulio la haraka ambapo Okwi akipokea mpira wa Kagere upande wa kushoto mwa goli la Leopards alimpiga chenga na kumuweka chini beki aliyekuwa akimkaba na kupiga pasi ya mwisho kwa Clatous Chama ambaye aliunganisha mpira huo moja kwa moja mpaka kwenye wavu na kuiandikia Simba bao la pili.
Leopards waliendelea kufanya mashambulizi ya kawaida lakini dakika 61 Oburu Vincent aliifungia timu yake bao la kufutia machozi.
Mara baada ya kupata bao Leopards walionekana kushambulia zaidi kuliko Simba lakini walikosa umakini hasa ndani ya 18 kila walipoingia.
Mpaka kipyenga cha mwisho cha mwamuzi, Godfrey Nkahakananga kutoka Malawi anapuliza Simba walishinda 2-1 na kutinga hatua ya nusu fainali ambapo watacheza na Bandari. Wakati huo huo, Chama aliibuka mchezaji bora na kuzawadiwa Dolla 500 (zaidi ya Sh 1 milioni).




0 Comments