Baada ya uongozi wa Simba kutangaza kuachana na kocha Patrick Aussems hapo jana, zoezi hilo litaendelea upande wa wachezaji ambapo nyota kadhaa wako hatarini kuachwa usajili wa dirisha dogo
Simba imetaja moja ya sababu ya kumuondoa Aussems ni kushindwa kuifikisha timu hatua ya makundi michuano ya ligi ya mabingwa msimu huu
Lakini Aussems nae alitoa malalamiko kuwa baadhi ya wachezaji waliosajiliwa hayakuwa mapendekezo yake
Miongoni mwa nyota hao ni wachezaji watatu raia wa Brazil Tairone Da Silva, Wilker na Fraga
Kuondolewa kwa Aussems ni dhahiri kutaongeza presha kwao kwani kwa muda waliokaa Simba hawajaonyesha 'maajabu'
Nyota hao wameonyesha viwango vya kawaida ambavyo havitofautiani sana na wachezaji wengi wa Kitanzania
Aidha inaelezwa Simba imedhamiria kukamilisha sehemu kubwa ya michakato yake ya usajili dirisha dogo ili mwezi Juni/Julai kusiwe na michakato mingi kama ilivyokuwa msimu huu
Uamuzi huu umesukumwa na mabadiliko ya kalenda ya CAF ambapo michuano ya ligi ya mabingwa inaanza mwanzoni mwa August
Moja ya changamoto zilizoikwamisha Simba kwenye michuano hiyo msimu huu ni ufinyu wa muda wa kufanya maandalizi wakati timu ikiwa imesajili nyota wengi
Hata hivyo uongozi wa Simba umeshauriwa kumaliza mchakato wa kumpata kocha ambaye ndiye anapaswa aachiwe majukumu ya kukiboresha kikosi chake
Na mchakato huo inafaa ukamilike haraka wakati huu ambao ligi imesimama ili kocha huyo apate muda wa kukifanyia tathmini kikosi kabla ya kutoa mapendekezo
0 Comments