Windows

Manara apigilia msumari kuondoka kwa Aussems



Afisa Habari wa klabu ya Simba Haji Manara amesema Bodi ya Wakurugenzi ililazimika kuchukua hatua ya kumfuta kazi kocha Patrick Aussems ili kurejesha hali ya utulivu ambayo ilikuwa imeanza kupotea

Manara amesema pamoja na kazi nzuri aliyoifanyia Simba, Aussems alikuwa na mapungufu ambayo ilikuwa vigumu kuendelea kuwa nae

Aidha, Msemaji huyo wa Simba amesisitiza kuwa uamuzi huo haukufanywa na Mtendaji Mkuu Senzo Mazingisa, ulifanywa na Bodi ya Wakurugenzi akiwemo Mwenyekiti wa Bodi hiyo Mohammed Dewji 'Mo'

Manara amesema ulifika wakati timu ilikosa umoja na kuwa hata ushindi ambao wamekuwa wakiupata katika michezo ya hivi karibuni umetokana na uwezo wa wachezaji

"Katika hili hapaswi kulaumiwa Mtendaji Mkuu Senzo Mazingisa kama wanavyofanya wachache. Bodi ya wakurugenzi ndiyo iliyofanya maamuzi, sio Senzo. Hakuna umoja ndani ya timu, timu imegawanyika. Tumefanya maamuzi ili kurekebisha hii hali. Timu ilikuwa inashinda kwa sababu ya uwezo binafsi wa wachezaji," amesema


Kukithiri kwa utovu wa Nidhamu

Manara amesema Aussems alishindwa kutimiza wajibu wake kusimamia nidhamu ya wachezaji na watendaji waliokuwa chini yake

"Viongozi hawakai na wachezaji kambini. Wajibu wa viongozi ni kuwaonya wachezaji na makocha kama kuna shida. Utovu wa nidhamu umekithiri, viongozi wamejitahidi lakini tabia hiyo inajirudia. Maamuzi haya ni kwa sababu kocha ameshindwa kusimamia nidhamu ya wachezaji"

Ubaguzi wa Wachezaji

Manara amesema Aussems alifanya ubaguzi wa wachezaji waziwazi. Hali hiyo ilipelekea kutengeneza makundi miongoni mwao

Aussems aliwagawa wachezaji makundi makuu mawili. Sasa kocha huwezi kuendesha timu hivyo. Juzi ametoka kumdhihaki mchezaji (Dilunga) bila sababu yoyote.

Manara amesema mashabiki wa Simba inapaswa wawe wamoja na kuunga mkono uamuzi uliofanywa na Bodi kwani ni kwa maslahi ya klabu

"Wapo wanaodhani waliofanya uamuzi huu hawipendi Simba. Sio kweli, yaani Mo Dewji haipendi Simba? Bodi ya wakurugenzi hawaipendi Simba? Haiwezekani Mo Dewji awekeze fedha zake halafu afanye maamuzi yasiyo na tija. Kama timu haina nidhamu haiwezi kusonga mbele"



Kwa habari zaidi Download App ya soka kiganjani kutoka Play Store.

Post a Comment

0 Comments