Windows

Hii Yanga kweli inautaka ubingwa wa ligi kuu





Sasa ni rasmi mshambuliaji Ditram Nchimbi anatua Yanga baada ya uongozi wa Azam Fc kuthibitisha kuwa tayari wamemalizana na Yanga

Nchimbi anatua Yanga wakati mwafaka kwani Januari 04 2020 mabingwa hao wa kihistoria watamuhitaji kwenye mchezo dhidi ya watani zao Simba utakaopigwa uwanja wa Taifa

Nchimbi anaungana na washambuliaji wengine David Molinga na Tariq Seif ambaye nae amesajiliwa hivi karibuni

Kwa wale waliokuwa wanadhani Yanga iliposema inautaka ubingwa msimu huu kuwa ni masihara, pole yao kwani mabingwa hao wa kihistoria wamedhamiria kwelikweli kuurejesha ubingwa Jangwani baada ya kuukosa kwa misimu miwili mfululizo

Nchimbi amepeleka mabao Yanga, kwani anajiunga na miamba hao wa soka Tanzania akiwa na mabao yake manne kwenye ligi

Ni idadi hiyo ya mabao pia amefunga mshambuliaji David Molinga 'Falcao'

Huku Molinga huku Nchimbi pale Tariq kazi ipo

Nchimbi ni aina ya washambuliaji ambao mabeki hawapendi kukutana nao kutokana na aina yao ya uchezaji

Ni mshambuliaji msumbufu, lakini pia anapouweka mpira mguuni ni vigumu kuupokonya

Aina yake ya uchezaji haitofautiani sana na Molinga pengine washambuliaji hao wanakwenda kutengeneza pacha hatari

Mshambuliaji Tariq Seif huenda akanufaika zaidi na uwepo wa washambuliaji hao kwani yeye kazi yake kubwa ni kufunga tu

Aina ya uchezaji wa Tariq unaweza kuifananisha na Amissi Tambwe



Ni mchezaji anayefahamu kujiweka katika mazingira ambayo yatampa nafasi ya kufunga

Ujio wa washambuliaji hao unakwenda kubadili kabisa taswira ya safu ya ushambuliaji ya Yanga

Nchimbi na Tariq ni wachezaji ambao wanaifahamu vyema ligi ya Tanzania Bara, hawatahitaji muda wa kuzoea mazingira kama ilivyokuwa kwa watangulizi wao Sadney Urikhob na Juma Balinya

Hawa wanaweza kuanza kuihesabia mabao Yanga mapema tu

Post a Comment

0 Comments