Azam ipo nafasi ya nne, mbele ya Mtibwa na Namungo ikifuata zikitofautishwa na uwiano wa mabao ya kufunga na kufungwa tu, lakini Yanga ikifunga mabao 11 na kufungwa saba hadi sasa.
MASHABIKI wa Simba huenda viroho vipo juu kwa sasa kutokana na kasi waliyonayo wapinzani wa jadi, Yanga ambao wameshinda mechi tano mfululizo katika Ligi Kuu Bara, huku pambano lao la kwanza la msimu huu likiwa karibuni.
Yanga jana ilipata ushindi wa mabao 2-1 dhidi ya Alliance kwenye Uwanja wa CCM Kirumba, jijini Mwanza na kuzidi kukwea kutoka eneo la chini wakipanda hadi nafasi ya 12 na kama keshokutwa Jumatatu watapata ushindi mbele ya KMC watakuwa na nafasi ya kuingia Tano Bora.
Kwa sasa mabingwa hao wa kihistoria wana pointi 16 na kama wakishinda mbele ya KMC ambao imekuwa na mwenendo mbaya tangu msimu uanze licha ya kumfurusha aliyekuwa kocha wao, Jackson Mayanja, itafikisha alama 19 na kulingana na timu za Azam, Mtibwa Sugar na Namungo.
Azam ipo nafasi ya nne, mbele ya Mtibwa na Namungo ikifuata zikitofautishwa na uwiano wa mabao ya kufunga na kufungwa tu, lakini Yanga ikifunga mabao 11 na kufungwa saba hadi sasa.
Simba, yenyewe ipo kileleni mwa msimamo ikiwa na alama 25 baada ya mechi 10 na ikiwa haina mchezo wowote mpaka Januari 4 watakapokuwa wenyeji dhidi ya Yanga, inayosaka ushindi mbele ya watani wao hao tangu mwaka 2016.
Yanga ilishinda mara ya mwisho mbele ya Simba katika Ligi Kuu Bara Februari 20, 2016 walipoilaza mabao 2-0 kwa mabao ya Amissi Tambwe na Donald Ngoma ambao wote kwa sasa hawapo klabuni hapo na baada ya hapo imechezea vipigo vitatu na kuambulia sare tatu katika mechi sita.
Misimu mitatu iliyopita, Yanga ilipata sare katika mechi zao za kwanza lakini zile za marudiano wamejikuta wakikumbana na vipigo, ikiwamo ya mwisho ya msimu uliopita wakati Meddie Kagere alipowanyamazisha mashabiki wa Jangwani kwa bao la dakika ya 71.
Simba na Yanga zitakutana kwenye mechi yao ijayo mwakani zikiwa zimetofautiana michezo miwili , Yanga ikimalizana na KMC itafikisha mechi nane, huku timu hizo zikiwa na makocha tofauti baada ya Yanga kumtimua Mwinyi Zahera na kuikabidhi timu kwa Charles Mkwasa, huku Simba ikiachana na Patrick Aussems.
Kocha Mkwasa jana alisema matokeo mazuri kwa timu yake yanatokana na vijana wake kufuata yale wanayoelekeza na sasa wanaufikiria zaidi mchezo dhidi ya KMC kabla ya kujipanga kwa mechi ya watani.
Tangu Yanga iwe chini ya Mkwasa imecheza mechi tatu za ligi na kushinda zote ikianza kwa kuifumua Ndanda bao 1-0 kisha kuilaza JKt Tanzania mabao 3-2 na jana kuinyuka Alliance 2-1.
Kocha maarufu na mchambuzi wa soka nchini, Kennedy Mwaisabula 'Mzazi' alisema mwenendo wa ushindi mfululizo kwa Yanga unazidi kuwapa kujiamini nyota wake, licha ya kukiri kwamba bado timu imekuwa ikitengeneza nafasi nyingi, lakini inashindwa kuzitumia kutokana na papara.
"Ushindi huu ni mzuri kwa Yanga, ikizingatiwa kuwa, bado wana michezo mingi mkononi, lakini ni lazima timu iwe inazitumia nafasi inazotengeneza," alisema Mzazi aliyeweahi kuinoa Yanga.
Matokeo ya watani tangu Okt 2016
Okt 01, 2016
Yanga 1-1 Simba
WAFUNGAJI: Amissi Tambwe 26', Shiza Kichuya 82'
Feb 25, 2017
Simba 2-1 Yanga
WAFUNGAJI: Simon Msuva 5' pen; Laudit Mavugo 66' na Shiza Kichuya 81'
Okt 28, 2017
Yanga 1-1 Simba
WAFUNGAJI: Obrey Chirwa 60'; Shiza Kichuya 57'
Apr 29, 2018
Simba 1-0 Yanga
MFUNGAJI: Erasto Nyoni 37'
Sept 30, 2018
Simba 0-0 Yanga
Feb 16, 2019
Yanga 0-1 Simba
MFUNGAJI: Meddie Kagere 71'
0 Comments