KATIKA mpira wa miguu kuna kikosi cha kwanza na cha pili, lakini pia huwa kuna wale wachezaji ambao wakiingia tu basi wanabadilisha mpira pindi wanapopewa nafasi.
Hilo lipo duniani kote kwamba si wote ambao wanaanzia nje, basi wanakuwa hawana kiwango bali watu ambao wanakabiliana nao ndio changamoto inayowafanya wakae nje.
Mwanaspoti limeangazia wachezaji ambao wanakaa benchi Ligi Kuu Bara lakini wakipewa nafasi tu wanafanya vizuri kiasi kwamba watu wanajiuliza inakuwaje wanaachwa nje.
MWADINI ALLY
Kipa huyu ana takribani miaka mitano akiwa Azam FC, wanaenda makipa wapya na kuondoka, wanaenda makocha wapya wanaondoka lakini yeye atabaki.
Mwadini amekuwa akikosa namba mbele ya Razack Abarola kwa misimu miwili, lakini akipewa nafasi hufanya vizuri.
Katika mechi dhidi ya Mbao FC mjini Mwanza, Mwadini aliokoa michomo mingi na kuiwezesha Azam FC kupata ushindi wa kwanza katika Uwanja wa CCM Kirumba baada ya kushindwa kufanya hivyo katika mechi mbili.
JUMA ABDUL
Hivi sasa beki wa kulia katika kikosi cha Yanga ni Paul Boxer, lakini baada ya kuumia tu Juma Abdul alipata nafasi ya kuanza kikosi cha kwanza. Abdul tangu amepewa nafasi ya kuanza katika kikosi hicho ameendelea kuonyesha kiwango bora hasa upande wa upigaji krosi ambazo zinasifika kuwa na macho. Beki huyo pia ameweza kuziba vizuri pengo la chipukizi Paul Godfrey ‘Boxer’ ambaye msimu uliopita alicheza kwa kiwango kikubwa baada ya kuaminiwa na aliyekuwa kocha mkuu, Mwinyi Zahera.
AMOS CHARLES
Beki huyo alisajiliwa msimu huu akitokea katika klabu ya Mbao FC na katika mechi za za Kagame Cup alikuwa anaanza, lakini katika upande wa Ligi Kuu ikageuka kuwa changamoto.
Amos amekosa nafasi mbele ya Ally Ramadhan ambaye amekuwa mwepesi katika kupiga krosi za uhakika kuelekea langoni hali iliyomfanya Charles kukaa pembeni. Lakini anapokuwa anapewa nafasi bado amezidi kuonyesha ukomavu wa kujituma na kupandisha mashambulizi licha ya kuwa na kasoro ndogondogo.
DANIEL AMOAH
Mwanzoni mwa msimu huu Amoah alianza kupata nafasi ya kuanza katika kikosi cha kwanza akiwa na Yakub Mohamed.
Hilo lilikuja baada ya beki Agrey Morris kupata majeraha ya goti yaliyomfanya akae nje mwanzoni mwa msimu huu. Baada ya kupona Aggrey, Amoah amerejea katika benchi lake na kuendelea kusugua kama kawaida, lakini si kwamba kiwango chake kimeshuka.
ALLY ALLY
Akiwa Stand United, KMC mpaka Yanga amezidi kuonyesha uwezo wake, anapokuwa yupo uwanjani katika beki wa kati.
Yanga ilipomsajili akitokea KMC wengi walishtuka, lakini alipokwenda katika kikosi hicho aliweza kuziba pengo la Lamine Moro pindi alipokosekana uwanjani au Kelvin Yondani.
Licha ya kutopata nafasi mbele ya Lamine, Yondani na Ally Abdulkarim ‘Sonso’, akipewa nafasi anaendeleza uwezo wa kucheza nafasi hiyo vizuri.
MASOUD ABDALLAH ‘CABAYE’
Jina la Cabaye alipewa kutokana na uwezo wake wa kukaba uwanjani. Hakuna ubishi kwenye uwezo wake wa kukaba yupo vizuri.
Masoud amekosa namba mbele ya Mudathir Yahya na hilo lilimfanya msimu uliopita kutoka kwa mkopo kwenda KMC.
Msimu huu amerejea Azam FC na amekutana upya na Mudathi, katika mchezo wa juzi dhidi ya Mbao FC ambapo kocha Aristica Cioaba alimpa nafasi ya kucheza sambamba na Mudathir na alionyesha uwezo wa hali ya juu katika ukabaji.
IDD KIPAGWILE
Anakumbukwa kwa namna ambavyo aliifanya Simba katika Kombe la Mapinduzi mwaka juzi, baada ya kutumia uwezo wake wa kupiga chenga vizuri.
Amekuwa hapati nafasi katika kikosi cha Azam mbele ya winga Joseph Mahundi hasa katika msimu uliopita na huu amekumbana na changanoto nyingine mbele ya Idd Seleman ‘Nado’.
Lakini anapopewa nafasi ya kucheza, Kipagwile amekuwa akicheza vizuri na kocha Cioaba ameanza kumpa nafasi baada ya kumpa dakika 70 katika mchezo dhidi ya Mbao FC.
MAPINDUZI BALAMA
Inawezekana kocha Zahera kuna kitu alikiona kwa Balama na kuamua kumchezesha kama beki wa kulia au winga wa kulia.
Lakini pia inawezekana kutokana na uwepo wa Feisal Salum na Mohamed Issa katika eneo la kiungo kulimfanya Balama acheze kama beki wa kulia na muda mwingine kukosa namba hasa baada ya Juma Abdul kurejea. Hivi sasa kaimu kocha mkuu Charles Mkwasa anampa nafasi katika kiungo na amezidi kuonyesha uwezo mkubwa.
SHABAN CHILUNDA
Amekosa nafasi ya kucheza mbele ya Donald Ngoma na Obrey Chirwa katika kikosi cha Azam, lakini anapopata nafasi ya kuitwa katika kikosi cha timu ya Taifa Tanzania ‘Taifa Stars’ anafanya mambo makubwa.
Licha ya kukosa nafasi, akiingizwa huwa anaonyesha kitu tofauti uwanjani hali inayotoa majibu kwamba, kukaa kwake nje haimaanishi kuwa hana uwezo.
Chilunda ni mchezaji mnyumbulifu na analijua goli vilivyo pindi anapokuwa yuko karibu na lango.
MOHAMED ‘MO’ RASHID
Simba wamemtoa kwa mkopo kwenda JKT Tanzania baada ya kukosa nafasi ya kucheza mbele ya washambuliaji Emmanuel Okwi, John Bocco na Meddie Kagere katika msimu uliopita. Licha ya kwenda katika kikosi hicho bado ameendelea kukosa namba mbele ya Abdulrahman Mussa na Adam Adam.
Mo akiwa anaingia akitokea benchi huwa anafanya kitu cha ziada hasa kuwasumbua mabeki na kukaa na mpira.
RASHID JUMA
Ni kijana mwenye spidi ya hali ya juu na uwezo mkubwa katika kumiliki mpira pindi anapokuwa yupo uwanjani.
Juma anatumika hasa katika kikosi cha Simba kwenye kipindi cha pili katika kuhakikisha anaendelea kuwasumbua mabeki wa timu pinzani.
0 Comments