


MABOSI wa Yanga tangu Jumatano usiku wapo Misri walipokwenda kuandaa kambi ya timu hiyo huku wakipata ushirikiano kutoka kwa mashabiki wa wapinzani wao Pyramids FC wa nchini humo.
Hiyo ni katika kuelekea mchezo wa marudiano wa Kombe la Shirikisho utakaozikutanisha timu hizo kesho Jumapili.
Wapinzani wa Pyramids kwenye Ligi Kuu ya Misri ni Al Ahly, Zamalek na Masry ambao wanatajwa kuungana kuisapoti Yanga watakapokuwepo uwanjani.
YANGA
Akizungumza na Championi Jumamosi, Makamu Mwenyekiti wa Yanga, Frederick Mwakalebela alisema kuwa, kwa upande wao wa viongozi wamejiandaa vizuri katika kuelekea mchezo huo mgumu ambao anaamini watapata matokeo mazuri.
Mwakalebela alisema yupo nchini humo tangu Jumatano kwa ajili ya kuandaa kambi na uwanja mzuri watakaofanya mazoezi kabla ya msafara wa timu hiyo kutua Misri juzi Alhamisi.
Aliongeza kuwa ana matumaini ya ushindi baada ya kupata taarifa nchini humo, Pyramids inazungumziwa kama timu ya kawaida, hivyo kama wachezaji wao wakipambana, basi watapata matokeo mazuri.
“Tangu nimefika hapa Misri, nimekuwa nikipata ushirikiano mkubwa kutoka kwa wapinzani wa Pyramids ambao wametupa maneno ya matumaini ya kupata matokeo mazuri.
“Na moja ya taarifa nzuri ni kuwa huku Misri inaonekana ni timu ndogo ya kawaida ambayo kama wachezaji wakipambana, basi hakuna kitakachotuzuia kupata ushindi ugenini.
“Hivyo, tunatarajia kuupata ushirikiano mkubwa kutoka kwa mashabiki wa timu pinzani wa Pyramids ambao wameonekana kutaka kutusapoti tutakapokuwa uwanjani,” alisema Mwakalebela.
The post Warabu Waiongezea Nguvu Yanga Iwaue… appeared first on Global Publishers.



0 Comments