Windows

LIVERPOOL, MAN U Zatinga Robo Fainali CARABAO Kibabe

LIVERPOOL ikiwa nyumbani kwao kwenye Uwanja wa Anfield usiku wa kuamkia leo Alhamisi, licha ya kupanga ‘vitoto’ vingi katika kikosi chao, lakini iliibuka na ushindi wa penalti 5-4 dhidi ya Arsenal na kutinga robo fainali ya michuano ya Kombe la Carabao.

Mchezo huo uliteka hisia za mashabiki wengi duniani kutokana na kufungwa jumla ya mabao 10 ndani ya dakika tisini zilizomalizika kwa matokeo ya 5-5.

 

Katika mabao hayo, Liverpool ndiyo ilikuwa ya kwanza kupata bao dakika ya sita baada ya beki wa Arsenal, Shkodran Mustafi kujifunga. Kiungo wa Arsenal, Lucas Torreira akasawazisha bao hilo dakika ya 19 akiuwahi mpira uliotemwa na kipa wa Liverpool, Caoimhin Kelleher, kisha Gabriel Martinelli alifunga bao la pili na la tatu kwa Arsenal dakika ya 26 na 36. Mzee wa penalti, James Milner akaifunga Liverpool bao la pili dakika ya 43 kwa mkwaju wa penalti. Timu hizo zikaenda mapumziko Arsenal ikiwa mbele kwa mabao 3-2.

Mesut Ozil ambaye katika mchezo huo alicheza kwa dakika 65 kabla ya kutoka, alitoa asisti kwa Ainsley Maitland-Niles aliyefunga bao la nne dakika ya 54. Alex Oxlade-Chamberlain na Divock Origi, walifunga mabao mawili ya harakaharaka kwa Liverpool dakika ya 58 na 62 na kufanya matokeo kuwa 4-4. Kisha Joseph Willock akaifunga Arsenal bao la tano dakika ya 70 na kufanya matokeo kuwa Arsenal 5 na Liverpool 4.

 

Ikiwa imebaki dakika moja kati ya tano zilizoongezwa baada ya zile tisini kumalizika huku Arsenal ikiamini kwamba imeshinda, Origi aliisawazishia Liverpool na kufanya matokeo kuwa 5-5. Timu zikaenda kwenye mikwaju ya penalti ambapo huko Liverpool haikufanya makosa.

Penalti za Liverpool zilizopigwa na James Milner, Adam Lallana, Rhian Brewster, Divock Origi na Curtis Jones zilijaa kimiani, huku Arsenal waliopata ni Hector Bellerin, Matteo Guendouzi, Gabriel Martinelli na Ainsley Maitland-Niles. Wakati Daniel Ceballos akikosa.

 

Katika mchezo mwingine wa michuano hiyo ambao uliteka hisia za mashabiki wengi uliochezwa usiku wa kuamkia leo, Manchester United iliichapa Chelsea mabao 2-1 kwenye Uwanja wa Stamford Bridge, nyumbani kwa Chelsea. Marcus Rashford aliifungia Manchester United mabao yote dakika ya 25 kwa penalti na dakika ya 73 kwa faulo.

 

Lile la Chelsea lilifungwa na Michy Batshuayi dakika ya 61. Ikumbukwe kuwa, Arsenal ilipokutana na Liverpool kwenye Premier, ilichapwa, huku pia Man United nayo ikiichapa Chelsea kwenye Premier. Aston Villa nayo jana iliichapa Wolves mabao 2-1 na kutinga robo fainali ya michuano hiyo.

The post LIVERPOOL, MAN U Zatinga Robo Fainali CARABAO Kibabe appeared first on Global Publishers.


Post a Comment

0 Comments