

Kocha mpya wa Azam FC, Aristica Cioaba, akiwa na mtangulizi wake, Etienne Ndayiragije. Wawili hao wamekutana makao makuu ya Azam FC (Azam Complex) wakiwa pamoja na Ofisa Mtendaji Mkuu, Abdulkarim Amin ‘Popat’, kukabidhiana kijiti, ikiwemo Ndayiragije kuwaaga wachezaji na kwenda kwenye majukumu yake mapya ya timu ya Taifa.
KLABU ya Azam imeingia mkataba wa mwaka mmoja na Kocha wao wa zamani Aristica Cioaba ambaye anachukua mikoba ya aliyekuwa Kocha wao, Etienne Ndayiragije, ambaye anatarajia kutangazwa kama Kocha Mkuu wa kudumu wa timu ya Taifa ya Tanzania ‘Taifa Stars’.

Kocha huyo raia wa Romania, aliyewahi kuinoa Azam FC misimu miwili iliyopita, ataanza majukumu yake mara moja tutakapokamilisha taratibu za vibali vyake vya kufanya kazi nchini.

Aidha, kama ilivyokuwa awali Cioaba, mwenye leseni ya juu ya ukocha ya UEFA Pro Licence, amerejea sambamba na Kocha wa viungo, Costel Birsan, aliyekuwa naye awali kipindi anaifundisha Azam FC.

Mara baada ya kuingia mkataba rasmi mapema leo Jumatatu, Cioaba ameishukuru Bodi ya Wakurugenzi na uongozi mzima wa Azam FC kwa kuendelea kuwa na imani naye.
“Naushukuru uongozi wa Azam FC kwa kuendelea kuwa na imani na mimi, kikubwa mimi sio mgeni hapa naijua timu, wachezaji wananijua na pia wanafahamu falsafa yangu, jambo kubwa ni kuendelea kuifanya timu kuwa juu pamoja na kushinda mataji,” alisema.

Ndayiragije anaenda timu ya Taifa, baada ya Bodi ya Wakurugenzi ya Azam FC kuridhia ombi la Shirikisho la Soka Tanzania (TFF) wanaomuhitaji awe kocha mkuu wa kudumu baada ya kufanya vizuri akiwa na kikosi hicho akiwa kocha wa muda.

Azam FC tunamtakia kila la kheri, Ndayiragije katika majukumu yake mapya akiwa Taif Stars, ambapo tutakuwa naye sambamba pale atakapohitaji kutoka kwetu msaada kwenye masuala yake kiufundi.
The post Azam Yamtangaza Kocha Mpya appeared first on Global Publishers.



0 Comments