Windows

Taifa Stars Lazima Ishinde Ugenini

TIMU ya taifa ya Tanzania, Taifa Stars, jana imejikuta ikipoteza mchezo wa kwanza wa raundi ya pili ya kufuzu Kombe la Afrika kwa Wachezaji wa Ligi za Ndani (Chan) dhidi ya Sudan, kufuatia kipigo cha bao 1-0.

 

Mchezo huo ulipigwa kwenye Uwanja wa Taifa, Dar huku ukihudhuriwa na mashabiki wengi lakini Stars ilishindwa kuibuka na ushindi. Stars ilianza mchezo huo kwa kasi ambapo walikosa bao la wazi kupitia kwa Ayoub Lyanga aliyeingia na mpira katika eneo la 18 kabla ya kupiga shuti ambalo liliokolewa na kipa wa Sudan kabla ya Lyanga kukosa tena bao kwa kichwa.

 

Stars waliendelea kulisakama lango la Sudan katika kipindi cha kwanza bila mafanikio kabla ya Sudan kufanya mabadiliko ya kumtoa Mohamed Mahamoud na kuingia Nazair Hamid dakika 32, hadi timu hizo zinakwenda mapumziko matokeo yalikuwa ni sare ya 0-0.

 

Katika kipindi cha pili Stars walianza kwa kasi kwa kuliandama lango la Sudan lakini hawakuweza kupata bao. Sudan walifunga bao pekee kupitia kwa Yasir Mozamil dakika ya 60 baada ya kufanya shambulizi la kushtukiza huku mabeki wa Stars wakijua ametoa.

 

Dakika ya 67 ilibaki kidogo Gadiel Michael aisawazishie Stars baada ya shuti lake kuokolewa akiwa ndani ya 18 kabla ya Stars kumtoa Lyanga na kuingia Miraj Athuman katika dakika 68.

 

Stars waliendelea kutafuta bao la kusawaisha lakini hawakufanikiwa hadi kipyenga cha mwisho kinapulizwa. Mzamiru Yassin nusura afunge lakini shuti lake liligonga mwamba dakika ya 71. Alitolewa dk ya 72 na kuingia Hassan Dilunga.

 

Sasa Stars inatakiwa kushinda kwa zaidi ya bao 1-0 mchezo wa marudiano ugenini utakaopigwa Oktoba 18, ili iende Cameroon kwenye michuano hiyo hatua ya makundi.

 

KIKOSI: Juma Kaseja, Boniface Maganga, Gadiel Michael, Erasto Nyoni, Kelvin Yondani, Salum Abubakar, Shaban Chilunda, Ayubu Lyanga, Mzamiru Yassin, Jonas Mkude na Idd Seleman.

The post Taifa Stars Lazima Ishinde Ugenini appeared first on Global Publishers.


Post a Comment

0 Comments