Windows

Simba Yaiteka Mara, ‘Biashara Waanza Kutimuana’

SIMBA wana mbwembwe sana. Baada ya timu yao kutua mjini Musoma jana wakasisitiza kwamba leo Biashara wanapigwa bao nne. Wanadai mechi ya kwanza ya msimu walikuwa wanajipanga na kuusoma mchezo ndio maana wakaruhusu bao moja kwenye ushindi wa mabao 2-1 dhidi ya JKT Tanzania.

 

Lakini hesabu zao sahihi walizianza kwenye mechi ya pili walivyoipiga Mtibwa mabao 2-0, mechi ya tatu wakamchapa Kagera mabao 3-0.

Na leo wametamba kwamba ni mechi ya nne ambayo itapendeza wakishinda mabao manne. Meneja wa Simba, Patrick Rweyemamu amesisitiza kwamba wako vizuri na sasa ni mwendo wa hesabu tu huku akiwasisitiza mashabiki wajae uwanjani leo kushangilia kwa kuhesabu pasi na mabao. Wenyeji Biashara United wamepoteza michezo mitatu na kuambulia pointi moja pekee.

 

Biashara hesabu zao kubwa ni kuvunja mwiko ambao msimu uliopita ulivunjwa na Simba kwa kufungwa mabao 2-0 na yote yakifungwa na nahodha John Bocco jambo lililowaumiza mashabiki.

 

Tayari kwenye michezo minne ambayo wamecheza mpaka sasa, safu ya ushambuliaji ya Biashara United imefunga bap moja tu jambo ambalo limefanya Kocha Msaidizi, Omari Madenge kupangua gia kuikabili Simba leo

KAGERE

Mshambuliaji wa Simba, Meddie Kagere ndiye mchezaji atakayekuwa analindwa leo na Biashara United kutokana na kasi yake ya kucheka na nyavu kwani ndani ya dakika 270 ambazo ni sawa na mechi tatu ametupia jumla ya mabao matano na akitoa asisti mbili.

 

VIKOSI Biashara; Kasembo Doulglas, Ally Mussa, Lambere Jerome, Justin Omary, Innoncet Edwin, Ramadhan Chombo, Derrick Mussa, Abdulmajid Mangalo, Wilfred Kouruma, Juma Mpakala na Msapi Nasibu.

Simba; Aishi Manula, Haruna Shamte, Mohamed Hussein, Tairone Santos, Pascal Wawa, Gerson Fraga, Francis Kahata, Mzamiru Yassin, Meddie Kagere, Said Ndemla na Sharaf Shiboub.

 

MAKOCHA Omary Madenge, Kocha msaidizi wa Biashara United alisema; “Msimu uliopita tuliambulia pointi moja kwa Simba, msimu huu tupo vizuri na lengo letu ni kuona tunapata pointi tatu muhimu. Matokeo ya mechi za nyuma hayahusiani na mechi ya Simba.”

Kocha Patrick Aussems anasema kwamba; “Mpango wetu ni uleule tunataka ushindi na tunataka tuwaonyeshe ubora wa Simba,ni mechi ngumu lakini tutacheza mpira wetu na tutashinda.”

 

Meneja Rweyemamu aliongeza kuwa; “Wachezaji wetu wako katika hali nzuri na tumejipanga kupata matokeo ya kufurahisha dhidi ya Biashara United ili tuweze kutetea ubingwa wetu kwa msimu wa tatu mfululizo.”

 

“Tukishinda michezo yetu ndiyo njia sahihi kwetu sisi ya kupata nafasi ya kucheza mashindano ya kimataifa, tuna kazi kubwa kama benchi la ufundi.”

 

“Tunaomba mashabiki waendelee kutuunga mkono kwa kuja kutushangilia, tutacheza vizuri kwa niaba yao,”alisisitiza kiongozi huyo mwenye ushawishi mkubwa ndani ya Simba.

 

TSHABALALA

Nahodha wa Simba, Mohamed Husein Tshabalala amesema; “Kazi yetu ni kuhakikisha tunashinda kila mchezo na tumejipanga kufanya hivyo na Biashara kikubwa tunawaomba mashabiki wetu wajitokeze kwa wingi uwanjani kutupa sapoti. Biashara haitakubali kufungwa kirahisi lakini tutapambana.”

The post Simba Yaiteka Mara, ‘Biashara Waanza Kutimuana’ appeared first on Global Publishers.


Post a Comment

0 Comments