Windows

Jicho la Mwewe: Simba haikumpata Kagere kutoka Brazil

Jicho la Mwewe,
MOJA kati ya maswali maarufu mitaani katika soka ni kuhusu Wabrazili wa Simba. ‘Vipi wana uwezo?’ ‘Vipi umewaona?’ ‘Vipi watatufaa?’. Haya ndio maswali ambayo mashabiki wamekuwa wakiulizana mitaani. Unaishia kutabasamu.\

Popote kwenye wasiwasi basi kuna tatizo. Kwa nini mashabiki wana wasiwasi? Nadhani hawaamini mchezaji anaweza kuvuka bahari kutoka Brazil, akazivuka nchi zote akatua Tanzania. Wengine hawaamini kama Mbrazili mwenye umri wa miaka 23 anaweza kutua Simba kama kweli ana uwezo wa kucheza soka katika kiwango cha juu.

Simba iliamua kuendeleza mwiko ambao umewahi kufanywa na Coastal Union na kisha Yanga kwa kuchukua wachezaji kutoka Brazil. Unapomchukua mchezaji kutoka Brazil unatengeneza mashaka kuhusu uwezo wake.
Kwa nini klabu kubwa barani Afrika hazina wachezaji kutoka Brazil? Zamalek, Al Ahly, Kaizer Chiefs, Orlando Pirates na nyinginezo. Ukweli, kulikuwa na kujionyesha ‘show off’ kwa kuchukua wachezaji kutoka Brazil.

Inawezekana ni wachezaji wazuri lakini gharama za kuwavusha kutoka walikotoka kuja kucheza Tanzania zinaweza kuwa kubwa kuliko kuendelea kusaka wachezaji kama Meddie Kagere kutoka ndani ya bara hilihili.

Bado kuna wachezaji wengi kutoka ukanda huu au ule wa kati au kule Afrika Magharibi ambao wangeweza kuifanyia Simba kazi nzuri kuliko kuleta mchezaji kutoka Brazil. Kama unaleta mchezaji kutoka Brazil nadhani inabidi awe mchezaji mzuri na muhimu kuliko wote waliobakia klabuni. Kama unachukua mchezaji kutoka Brazil lakini Kagere na John Bocco wanaendelea kuwa wachezaji muhimu zaidi klabuni basi ujue kuna tatizo. Lakini pia kina Kagere hawahitaji kuelekezwa sana kuhusu soka la Afrika.

Hawa kina Kagere wanavifahamu viwanja vyetu vibovu, wanafahamu mashabiki wanataka nini, wanafahamu hali ya hewa, wanafahamu tofauti ya kucheza na timu kutoka Misri na tofauti ya kucheza na timu kutoka DR Congo.

Kitu cha msingi kwa Simba na timu zetu zenye uwezo wa kipesa ni kuendelea kutanua wigo wa kuskauti wachezaji. Wakati huu michuano mbalimbali ya Afrika ikiendelea ni wakati sahihi zaidi wa klabu kutuma watu wao katika mechi mbalimbali kwa ajili ya kuangalia vipaji vya Kiafrika ambavyo vinaweza kumudu soka la Kiafrika.
Kwa mfano, baadhi ya mabosi wa Simba walipaswa kuwepo uwanjani pale Zambia kutazama mechi kati ya Zesco na Zanaco. Unaweza kuambulia wachezaji wawili watatu kwa ajili ya kuwafikiria katika dirisha kubwa la msimu ujao.
Kama KCC ya Uganda inacheza na Hearts of Oak ya Ghana pale Kampala, sio mbaya kwa timu zetu kutuma watu wao wa kuangalia mechi hiyo.
Hiki ni kitu ambacho tumekuwa hatukifanyi. Mara nyingi klabu zetu zimekuwa zikianza kusaka wachezaji wakati wa dirisha la usajili linapofunguliwa. Hatuwezi kufanya uwezekezaji mpaka labda mchezaji mwenyewe ajilete nchini na klabu yake. Kwa mfano, bila ya michuano ya Chalenji iliyowahi kufanyika hapa nchini ina maana Azam isingewaona mastaa wake maarufu wa zamani, Kipre Tchetche na Kipre Balou. Kwa nini sasa hivi wanashindwa kutuma watu wao kwenda kutazama kinachoendelea Ligi za Ivory Coast, Ghana, Mali na kwingineko?
Yanga isingecheza na Platinum ya Zimbabwe ina maana isingewaona kina Thaban Kamusoko na Donald Ngoma. Au vipi? Kwa nini mabosi wetu hawaifuatilii Ligi Kuu ya Zimbabwe na kujua kinachoendelea?
Simba iliwaona wapi Wabrazili wake kabla ya kuwanunua? Nani aliwafuatilia? Kitu ambacho unaweza kuambiwa, viongozi walitazama mikanda yao. Ukwelihakuna mchezaji mbaya katika ‘highlight’. Vinakatwa vipande ambavyo mchezaji anacheza mzuri katika video hizi mchezaji wa kawaida anaweza kuonekana Lionel Messi. Mfumo wetu wa kununua mastaa bado ni wa kubahatisha. Kama tukituliza kichwa bado kuna wachezaji mahiri katika ukanda huu huu ambao wanaweza kutengeneza kikosi kabambe ambacho kinaweza kuzifanya klabu zetu kuwa tishio.
Mpira wa Afrika Mashariki umekuwa na hakuna haja ya kuvuka bahari za Pacific wala Atlantic kwa ajili ya kununua wachezaji.
Tuendelee kuwaombea mastaa wa Kibrazili wa Simba wafanye kazi nzuri lakini sidhani kama Simba iliwahitaji sana kwa sasa. Kagere hakutoka Brazil. Kuna kina Kagere wengine wengi katika mitaa ya nchi mbalimbali ya barani Afrika.

Post a Comment

0 Comments