Windows

Da Silva safari ya Wawa ndo imefika mwisho Simba

Da Silva safari, ya Wawa ndo imefika, mwisho Simba, Mwanaspoti, TanzaniaKWA muda mrefu sasa, safu ya ulinzi ya Simba imekuwa ikiundwa na mabeki wawili wa kati, Pascal Wawa kutoka Ivory Coast na mzawa Erasto Nyoni.
Hata hivyo, baada ya Simba kuruhusu mabao matatu kwenye mechi mbili mfululizo dhidi ya timu za Azam FC na UD Songo, iliamua kufanya mabadiliko kwenye kikosi chake kilichocheza mechi ya kwanza ya Ligi Kuu dhidi ya JKT Tanzania. Miongoni wa mabadiliko hayo ni kumpumzisha Wawa na kumuanzisha beki kutoka Brazil, Tairone da Silva kucheza sambamba na Nyoni.
Silva alionyesha kiwango kizuri kwenye mechi hiyo na hapana shaka kama atapata nafasi ya kutosha ya kucheza, atakuwa mmoja wa mihimili ya Simba siku za usoni.
Lakini, ni wazi kwamba kwa kiwango chake dhidi ya JKT Tanzania, beki huyo anaiweka rehani nafasi ya Wawa kwenye kikosi cha kwanza. Makala hii inakuletea tathmini ya kwa nini Silva anaweza kuchukua nafasi katika kikosi cha kwanza  badala ya Wawa.

Stamina
Beki huyo ameonyesha kuwa fiti zaidi kuliko Wawa. Ni vigumu kwa mchezaji wa timu pinzani kumpora mpira pindi anapoumiliki na mapambano yote ya kimwili dhidi ya wachezaji wa JKT Tanzania alifanikiwa kuyashinda.
Ni tofauti na Wawa, ambaye katika siku za hivi karibuni amekuwa akipata wakati mgumu kuwadhibiti washambuliaji wenye nguvu.

Uwezo wa kupiga vichwa
Moja ya matatizo yanayoikabili Simba ni safu yake ya ulinzi kuwa dhaifu katika kuokoa mashambulizi ya mipira ya krosi, kona na ile ya juu. Mfano ilikuwa kwenye mechi dhidi ya AS Vita ya Ligi ya Mabingwa Afrika msimu uliopita ambapo, ilifungwa mabao mawili ya namna hiyo ilipopokea kichapo cha mabao 5-0 ugenini.
Lakini, angalau kidogo tatizo hilo limepata unafuu kutokana na uwepo wa Tairone, ambaye ameonyesha uwezo wa hali ya juu kuokoa mipira ya aina hiyo. Beki huyo ni mrefu kuliko Wawa kwani ana kimo cha Mita 1.91 ambao amekuwa akiutumia vyema kulinganisha na beki huyo wa Ivory Coast ambaye ana kimo cha Mita 1.78

Kushambulia
Kimo hicho cha Tairone sio tu amekuwa akikitumia kuokoa bali hata kushambulia, ambapo ameonyesha uwezo wa kupiga vichwa pindi Simba inaposhambulia kupitia kona au mipira ya faulo. Vichwa vyake vinalenga lango kwa usahihi tofauti na Wawa, ambaye hajawahi kuonyesha mchango mkubwa katika kushambulia kwa kutumia mipira ya juu.

Nidhamu, uungwana
Changamoto nyingine inayomkabili Wawa ni kucheza rafu zisizo na sababu, lakini pia amekuwa na hulka ya kuwafokea marefa na hata wachezaji wenzake. Lakini, Silva amekuwa akicheza kwa nidhamu na amekuwa akicheza rafu pale anapolazimika kufanya hivyo, lakini pia huwa sio mchezaji wa kubishana na waamuzi.

Kuchezesha timu
Kama ilivyo kwa Wawa, ambaye anaweza kuichezesha timu kutokea nyuma, hata Da Silva ameonyesha uwezo huo.
Beki huyo amekuwa akichezesha timu kutokea nyuma kwa kupiga pasi ndefu ambazo zimekuwa zikiwafikia walengwa kwa usahihi.

Maoni ya wadau
Kiungo wa zamani wa Kariakoo Lindi, Jemedari Said alisema Da Silva kama atapata nafasi ya kutosha ya kucheza ataisaidia Simba
“Ameonekana ana nguvu na hiyo ni sifa ya msingi ya beki na pia amekuwa akipiga pasi sahihi huku akifanya mambo ya msingi uwanjani. Anaweza kuwa na msaada kwa Simba kama atarekebishwa baadhi ya kasoro,” alisema.
Beki za zamani wa Simba, Boniface Pawasa alisema Da Silva anawapa changamoto mabeki wa kati wa Simba.
“Hofu yangu kwake ni umri tu, lakini namuona ni mchezaji anayeweza kutubeba kama atapata muda kidogo wa kuzoea mazingira na soka letu. Nimemuona ni aina ya mchezaji ambaye anacheza kwa ‘principal’ (misingi) za kimpira. Mfano huwa wa kwanza kufika katika mpira na kuuokoa.
Kwa namna ninavyofahamu kariba ya wachezaji wa Kibrazil na nilivyomtazama dhidi ya JKT, naamini tumepata mchezaji mzuri,” alisema.

Post a Comment

0 Comments