BAADA ya kiungo mpya wa Bayern Munich, Philippe Coutinho kupewa nafasi katika kikosi cha kwanza juzi kwenye mchezo wa Ligi Kuu Ujerumani dhidi ya Mainz, amewaahidi makubwa mashabiki kwenye michezo inayofuata.
Mchezaji huyo raia wa nchini Brazil aliyejiunga na kikosi hicho wiki moja iliopita akitokea Barcelona kwa mkopo, amedai atahakikisha mashabiki wanafuraia uwepo wake.
Amejiunga na mabingwa hao baada ya kushindwa kuonesha ubora wake Barcelona tangu alipojiunga akitokea Liverpool kwa rekodi ya usajili wa pauni milioni 145.
“Kwenye kikosi hiki kuna wachezaji wengi ambao ukicheza nao lazima utakuja kuwa bora, nina furaha kubwa kuwa hapa na ninaamini nitajifunza mengi kutoka kwao na nitakuwa mchezaji bora.
“Lengo kubwa ni kuisaidia timu kutimiza malengo, nitahakikisha ninafanya vizuri katika kila mchezo ambao nitapata nafasi ya kucheza,” alisema mchezaji huyo mara baada ya Bayern kushinda mabao 6-1.
Kocha wa timu hiyo Niko Kovac amedai atahakikisha anampa nafasi mchezaji huyo kwa ajili ya kuonesha kipaji chake kwa kuwa ni mmoja kati ya wachezaji wenye uwezo mkubwa katika safu ya kiungo.
“Lengo letu ni kumjenga mchezaji huyo, tutampa nafasi ili aweze kuonesha kipaji chake. Katika michezo ambayo amepata nafasi ameonesha kiwango kizuri na ameonesha kuwa ana kitu cha kuweza kuisaidia timu.
“Anajua jinsi ya kutengeneza nafasi, tunajua kwa sasa hayupo fiti kwa asilimia 100, hivyo katika michezo ijayo tutampa nafasi ya kucheza ndani ya dakika 60 hadi 70 na kwa kufanya hivyo tunaamini atarudi kwenye ubora wake,” alisema kocha huyo.
Mbali na Bayern Munich kushinda mabao 6-1, lakini wanashika nafasi ya pili kwenye msimamo wa Ligi baada ya kucheza michezo mitatu na kushinda miwili huku wakitoa sare mmoja, huku wakiongozwa na Red Bull Leipzig wenye pointi tisa baada ya kushinda michezo yote mitatu.
0 Comments