KOCHA Mkuu wa Yanga, Mwinyi Zahera, amefurahishwa na kiwango cha straika wake, Mnamibia, Sadney Urikhob, akikiri iwapo atapunguza kilo mbili, atakuwa mtamu balaa.
Kama hiyo haitoshi, Zahera alitoa siri jinsi alivyoizidi ujanja Simba kwa straika wake huyo.
Sadney ni miongoni mwa usajili mpya wa Yanga na juzi katika mchezo wa kilele cha Wiki ya Wananchi dhidi ya Kariobang Sharks ya Kenya kwenye Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam, alicheza dakika zote 90.
Katika mchezo huo, Wanajangwani hao walitoka sare ya bao 1-1, lakini mashabiki waliondoka roho kwatu kutokana na kiwango kilichoonyeshwa na nyota wao.
Sadney ni kati ya wachezaji waliokuwa kivutio katika mchezo huo, licha ya kwamba alikosa nafasi nyingi, akionekana kuelekea kuwalaza na viatu mabeki wa timu pinzani msimu ujao.
Zahera amethibitisha kiwango cha nyota huyo na kusema nguvu alizonazo, zinamwezesha kupambana na mchezaji yeyote uwanjani.
Alisema kuwa mshambuliaji huyo hana muda wa kumchenga mtu, bali akiona kuna anayetaka kumtibulia mipango yake, anatumia nguvu zake kumweka pembeni na kusonga zake mbele.
Zahera alisema upungufu alioonyesha nyota Sadney katika mchezo wa juzi ulitokana na kutokuwa na kuchelewa kujiunga na wenzake kambani, kwa takribani siku 10.
“Katika mchezo wa leo (juzi), Sadney angeweza kufunga mabao mawili, lakini miguu yake imeonekana kuwa mizito, nitakachofanya nitahakikisha anapungua kilo mbili na mtaona mbio zake.
“Kwa nilivyomuona, aina ya uchezaji wake, hana muda wa kumchenga mchezaji, akiwa na mpira, yeye anakubeba anakuweka huko naye anapita,” alisema Zahera.
Akizungumzia jinsi alivyompata mchezaji huyo, Zahera alisema baada ya kuonana naye katika michuano ya SportsPesa, wakati akifanya majaribio Simba, walianza kuwasiliana.
“Nilimuona Sadney katika SportsPesa, tukaanza kuwasiliana na kuwa marafiki na mwisho wa siku tukamsajili kwa sababu ni mchezaji mzuri, alinivutia,” alisema Zahera.
Kwa upande wake, Sadney alisema amefurahishwa na jinsi mashabiki wa Yanga walivyojitokeza uwanjani katika mechi yao ya kwanza, hivyo atajituma zaidi ili kuwapa furaha.
“Nimefurahishwa na jinsi mashabiki wa Yanga walivyo na mapenzi na sisi, nimenigusa, nitajitahidi kwa uwezo wangu kuwa bora zaidi ya kile nilichoonyesha,” alisema Sadney.
0 Comments