

Baada ya maboresho ya kikosi chake, kocha Mkuu wa Yanga Mwinyi Zahera amesema msimu huu watawania kutwaa ubingwa katika kila mashindano watakayoshiriki
Yanga ilimaliza nafasi ya pili kwenye ligi msimu uliopita nyuma ya Simba iliyotwaa ubingwa kwa tofauti ya alama sita
Mabingwa hao wa kihistoria pia waliishia kwenye hatua ya nusu fainali michuano ya kombe la FA
Hata hivyo msimu uliopita ulikuwa wenye changamoto nyingi kwa kikosi cha Yanga
Lakini Zahera amesema baada ya maboresho, msimu huu wanataka kutwaa ubingwa wa michuano yote
"Kwenye ligi tulimaliza nafasi ya pili msimu uliopita, msimu huu tunataka tuwe wa kwanza," amesema
"Kombe la FA tulitolewa hatua ya nusu fainali, msimu huu tunahitaji kufika fainali na kuweza kutwaa ubingwa"
Aidha kwa upande wa michuano ya ligi ya mabingwa, Yanga imeanza kampeni yake kwa kuchechemea baada ya kulazimishwa sare ya bao 1-1 na Township Rollers kwenye mchezo wa kwanza
Hata hivyo Zahera amesema wanaweza kupata matokeo mazuri kwenye mchezo wa marudiano nchini Botswana na kuweza kufuzu kwenda raundi ya kwanza



0 Comments