Windows

Yanga yapewa siri nzito




MSHAMBULIAJI wa Mtibwa Sugar aliyewahi kukipiga katika kikosi cha Zesco United ya Zambia, Juma Luizio, amesema Yanga hawana haja ya kuwa na wasiwasi kwani timu yake hiyo ya zamani kwa sasa si ya ushindani kama ilivyokuwa awali.

Yanga inatarajia kukutana na Zesco katika mchezo wa raundi ya kwanza ya Ligi ya Mabingwa Afrika, Septemba 14, mwaka huu kwenye Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam, ikiwa ni baada ya kuitoa Township Rollers hatua ya awali.

Akizungumza na BINGWA jana, Luizio alisema kuwa Zesco ya zamani ilikuwa na wachezaji mahiri kama Lazarous Kambole ambaye alikuwa ndiye tegemeo lao, lakini kwa sasa imekuwa ya kawaida.

“Zesco ilikuwa zamani sio sasa, miaka miwili iliyopita, ukitajiwa timu hiyo, unaanza kuwafikiria wachezaji kama Kambole ambaye alikuwa mzuri wa kucheka na nyavu.

“Yanga wajipange tu na kujua wanakutana na timu inayofanana mpira na wao, kitu pekee kitakachowapa ushindi ni umakini, lakini wasiwaze kama kuna wachezaji wa kuwasumbua sana,” alisema.

Yanga inakutana na Zesco United baada ya kuwatoa Township ya Botswana kwa jumla ya mabao 2-1, wakianza na sarea ya 1-1 nyumbani kabla ya kupata ushindi wa bao 1-0 ugenini.

Post a Comment

0 Comments