KOCHA Mkuu wa KMC, Jackson Mayanja, amelia na wimbi la majeruhi katika kikosi chake, huku mtangulizi wake, Etienne Ndayiragije, akimpa mbinu za kukifanya kuwa tishio Ligi Kuu Tanzania Bara.
KMC juzi ilicheza na Azam katika mchezo wao wa kwanza wa Ligi Kuu Tanzania Bara na kufungwa bao 1-0 kwenye Uwanja wa Uhuru, Dar es Salaam ambapo Mayanja alisema wimbi la majeruhi limekuwa likimpa wakati mgumu kusuka timu ya ushindani.
Mechi hiyo ilikuwa ya pili kwa KMC kupoteza mfululizo baada ya ile ya Kombe la Shirikisho Afrika waliofungwa na AS Kigali mabao 2-1 kwenye Uwanja wa Taifa, jijini.
Akizungumza na BINGWA jana, Mayanja alisema hajapata muda mzuri wa kukaa na wachezaji wake kutengeneza kikosi, huku wengine wakiwa wanakabiliwa na majeraha.
Alisema asilimia kubwa ya wachezaji majeruhi ni wale wa safu ya ushambuliaji, wakiwamo Salim Aiyee, James Msuva na Charles Ilanfya.
“Hata Vitalis Mayanga na Serge Alain, waliocheza leo (juzi), hawako vizuri, nimefanya kuwalazimisha, hali hiyo ndiyo inayoniumiza na kuifanya timu kupata matokeo mabaya,” alisema.
Mayanja alisema kutokana na kuondoka kwa wachezaji wengi waliokuwapo msimu uliopita katika kikosi cha kwanza, bado anafanya kazi kubwa kuijenga timu upya japo muda umekuwa ni mdogo.
Katika kuonyesha jinsi anavyogushwa na timu hiyo aliyokuwa akiinoa kabla ya kutua Azam, baada ya mchezo wao, Ndayiragije ‘alimvuta chemba’ Mayanja na kuteta naye, akimsisitiza mambo kadha wa kadha jinsi ya kukiongezea makali kikosi hicho cha Kinondoni.
0 Comments