Windows

Aussems amuuzia kesi Ajib



MABINGWA wa Ligi Kuu Tanzania, Simba, wanashuka dimbani leo JKT Tanzania kwenye Uwanja wa Uhuru, Dar es Salaam, kuanza mbio za kutetea taji lao, huku Ibrahim Ajib akibebeshwa jukumu la kupeleka furaha Msimbazi.

Simba wanaanza ligi hiyo, wakiwa na hasira za kuondolewa katika michuano ya Ligi ya Mabingwa Afrika ambayo msimu uliopita walifika hadi robo fainali.

Wanamsimbazi hao walikatishiwa safari yao ya kimatiafa msimu huu na UD Songo ya Msumbiji baada ya kupata suluhu ugenini, kisha kulazimishwa sare ya 1-1 kwenye Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam, wiki iliyopita.

Kutokana na hali hiyo, Simba wameamua kuelekeza nguvu zao zote katika ligi, wakipania pointi tatu leo ili kutetea ubingwa wao kwa mara ya tatu, lakini pia wakipigia hesabu Kombe la Shirikisho la Azam.

Licha ya kuwa na machungu ya kutolewa kimataifa, habari njema kwa Wanasimba ni kwamba leo katika kikosi cha kwanza wataanza kumuona Ajib aliyetua katika kikosi chao mwishoni mwa msimu uliopita akitokea Yanga.

Ajib alikosekana katika mechi zote mbili za kimataifa za Simba na ile ya Ngao ya Jamii dhidi ya Azam FC kutokana na majeraha yaliyokuwa yanamsumbua.

Katika mazoezi ya mwisho yaliyofanyika jana kwenye viwanja vya Gymkhana, Dar es Salaam, Kocha Mkuu wa Simba, Patrick Aussems, alionekana kusuka kikosi chake, huku kukiwa na mabadiliko makubwa.

Mbali ya Ajib aliyejumuishwa katika kikosi cha kwanza mazoezini, wengine ni Wabrazil wawili, Gerson Viera na Tairone Santos da Silva.

Hamu ya mashabiki wa Simba katika mchezo wa leo ni kuona wanapata ushindi mnono ambao utawaondolea machungu na kejeli za watani wao wa jadi Yanga baada ya kutolewa Ligi ya Mabingwa Afrika.

Katika mchezo wa leo, Simba wanajivunia rekodi zao kwa kuvuna pointi zote sita katika michezo miwili waliyokutana na JKT Tanzania msimu uliopita.

Simba ilianza kuibuka na ushindi wa mabao 2-0 dhidi ya JKT Tanzania katika mchezo wa mzunguko wa kwanza uliochezwa Novemba 2, mwaka jana, Uwanja wa Uhuru, Dar es Salaam kabla ya kuwachapa maafande hao bao 1-0 waliporudiana April 30, mwaka huu, kwenye uwanja huo.

Hata hivyo, Wekundu wa Msimbazi ha oleo watamkosa mshambuliaji wao, John Bocco ambaye anasumbuliwa na majeraha ya goti aliyoyapata katika mchezo wa Ngao ya Jamii dhidi ya Azam FC na Jonas Mkude anayeumwa na homa.

Akizungumzia mchezo huo, Aussems, alisema hakuna cha kupoteza kwa sababu ndiyo michuano waliyobaki nayo.

“Malengo yetu kwa sasa ni kufanya vizuri kwenye ligi, ni kitu pekee tulichobaki nacho na kitakachowafurahisha mashabiki wetu tukifanya vizuri,” alisema.

Kwa upande wake, Kocha wa JKT Ruvu, Abdallah Mohammed ‘Bares’, alisema anafahamu Simba itaingia katika mechi hiyo kwa nguvu zote kusaka ushindi, lakini hata yeye amejipanga hasa.

“Tunafahamu ugumu wa mchezo ulio mbele yetu, nafahamu ubora wa kikosi cha Simba na maumivu wanayopitia kutokana na matokeo waliyopata katika mchezo dhidi ya UD Songo, hasira zao zote sasa watazielekeza huku, ila wafahamu nasi tumejipanga,” alisema Bares.

Post a Comment

0 Comments