KUREJEA kwa Vodacom kama mdhamini mkuu wa Ligi Kuu Tanzania Bara, hakujaleta neema kwa klabu pekee, bali hata kwa wamuuzi ambao wanatarajiwa kulipwa madeni yao ya msimu uliopita kabla ya Oktoba mwaka huu.
Katika Ligi iliyopita, Shirikisho la Soka Tanzania (TFF), lilishindwa kuwalipa waamuzi waliochezesha mechi za Ligi Kuu Bara msimu uliopita kutokana na kukosekana kwa fedha.
Hadi ligi inamalizika, waamuzi walikuwa wamelipwa fedha za posho za mechi za mzunguko wa kwanza, hivyo TFF kubakiwa na madeni.
Akizungumza na BINGWA jana, Mwenyekiti wa Chama cha Waamuzi wa Soka Tanzania (FRAT) ambaye pia ni Mwenyekiti wa Kamati ya Waamuzi, Joseph Mapunda, alisema kuwa tayari kumefanyika uhakiki wa madeni yaliyopita lengo likiwa ni kuyalipa.
“Awali ilishindikana kuwapa waamuzi posho zao kwa wakati kwa sababu hakukuwa na mdhamini, jambo lililosababisha kuwepo na mlundikano wa madeni.
“Lakini baada ya kurejea kwa Vodacom, nimepewa maagizo ya kuwasiliana na waamuzi wenye madeni na kuwataka wafanye uhakiki ili waweze kulipwa.
“Kwa taarifa niliyopewa na TFF, waamuzi wote waliochezesha mechi msimu uliopita, watalipwa kabla ya kufika Oktoba mosi mwaka huu, hii ina maana zoezi hilo litafanyika mwezi mzima wa Septemba, hili ni jambo la faraja kwetu,” alisema.
Mbali ya hilo, Mapunda aliongeza kuwa TFF imewahakikishia msimu huu hakutakuwa na ucheleweshwaji wa malipo ya waamuzi kwa sababu tayari wameshaweka mipango mizuri ya upatikanaji wa fedha za malipo yao.
0 Comments