Timu za Simba na Yanga zimefanya usajili wa wachezaji wa kigeni kwenye vikosi vyao lakini kila timu imewapa nafasi nyota wao vile wanaweza.
Yanga hadi sasa imeipiga bao kwa wachezaji wa kigeni kuingia haraka katika kikosi cha kwanza kulinganisha na Simba ikitamba zaidi na wale wa zamani.
Iko hivi, Yanga imefanya usajili wa wachezaji tisa wa kigeni wakati Simba iliwanasa sita kutoka mataifa mbalimbali.
Yanga imewasajili, Wanyarwanda Issa Bigirimana (APR Rwanda), Patrick Sibomana (Mukura Victory Rwanda), Mrundi Mustapha Suleiman (Aigle Noir AC Haiti) na Mnamibia Sadney Ukhrob.
Wengine ni Mghana Lamine Moro, Mzambia Kalengo Maybin (Zesco), Juma Balinya raia wa Uganda, Mkenya Farouk Shikalo na Mkongo David Moringa 'Ndama' ambao wameungana na nahodha Papy Tshishimbi.
Wakati Simba wao wamewaongeza Wabrazil watatu Wilker Henrique Da Silva, Gerson Fraga na Tairone Da Siva, Mkenya Francis Kahata kutoka Gor Mahia, Mkongo Deo Kanda alikuwa TP Mazembe na Msudan Sharaf Shiboub.
Katika usajili huo mpya Yanga wamekuwa wakiwatumia wachezaji wao wapya kwenye kikosi cha kwanza huku wale wa zamani wakianzia benchi.
Ingizo jipya la wachezaji hao wa Yanga, limewafanya wale wazawa ambao kwa sasa ni wazawa kama Mrisho Ngassa, Deus Kaseke ambao msimu uliopita walikuwa na nafasi lakini sasa wanatokea benchi.
Achana na wa kigeni, wachezaji wazawa wapya wa Yanga wameingia na kuaminika kikosi cha kwanza kama kipa Metacha Mnata na Muharami Issa 'Marcelo' wanawaweka benchi Ramadhan Kabwili na wengine.
Hii kwa Simba ni tofauti kwani wakale wanawasubirisha wale wapya. Kwenye kikosi cha kwanza cha Simba ingizo jipya unaoweza kuwaona ni Kahata, Shiboub pamoja na Kanda ambaye pia hana nafasi katika kikosi cha kwanza.
Beki wa zamani wa Simba na Taifa Stars, Victor Costa ametolea ufafanuzi suala hilo na kusema ni muda.
"Kitu cha kwanza ni mipango ya mwalimu anataka kuwatumia wachezaji hao katika kipindi gani. Mfano Simba kuwatumia wengi wa zamani huenda anaona hawajawa na muunganiko mzuri hivyo anaona jambo zuri ni kuwapa muda,"alisema Costa.
"Kwa upande wa Yanga huenda kocha (Mwinyi Zahera) anaona kwake inafaa kuwa watampa matokeo mazuri ndio maana ameamua kuwapa nafasi zaidi hao wapya."
Alisema, kwa ujumla timu zote zimefanya usajili wa wachezaji wapya wa kigeni wazuri.
0 Comments